VIDEO: Majaliwa amkalia kooni mkurugenzi manispaa Iringa ujenzi wa ukumbi eneo la shule

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amempa saa nne mkurugenzi wa manispaa ya Iringa, Himid Njovu kuandika barua ya kusitisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano na sherehe unaojengwa katika eneo la Shule ya Msingi Gangilonga.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amempa saa nne mkurugenzi wa manispaa ya Iringa, Himid Njovu kuandika barua ya kusitisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano na sherehe unaojengwa katika eneo la Shule ya Msingi Gangilonga.

Ametoa agizo hilo leo Jumamosi Septemba 28, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Majaliwa ametaka kusitishwa kwa mkataba mtu aliyekodishwa eneo hilo na kisha lizungushiwe uzio, akisisitiza kuwa ni eneo la shule.

“Mkurugenzi kafute mikataba yote ya ujenzi wa miradi katika eneo la Shule ya Gangilonga pamoja na shule ya Wilolesi kwa sababu maeneo hayo hayaruhusiwi kujengwa miradi isiyohusiana na elimu. Eneo hilo lisafishwe na ujengwe uzio,” amesema Majaliwa.

Kabla ya Majaliwa hajatoa agizo hilo, mwanasheria wa Manispaa ya Iringa,  Nicholous Mwasungura amesema aliandaa mkataba wa kupangisha eneo hilo  kwa maelekezo ya kamati ya fedha,  Majaliwa kumuuliza kwa nini hakuwashauri kuhusu suala hilo kwa sababu tayari Serikali ilishatoa waraka wa kuzuia jambo hilo.

Awali, mkuu wa Mkoa wa Iringa,  Ally Happi aliwaonya watumishi kutojihusisha na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kuacha chuki, ubinafsi na roho mbaya na badala yake washikamane na wafanye kazi wa bidii.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera ameiomba Serikali izisaidie halmashauri za wilaya hiyo vyombo vya usafiri kwa sababu magari mengi ni chakavu hali inayosababisha mkurugenzi wa manispaa awe anaomba lifti kwake.

Akijibu suala hilo, Majaliwa amewataka waombe kibali cha ununuzi wa magari na watumie fedha zao za ndani.