VIDEO: Makamba, Kinana waliamsha ‘dude’

Monday July 15 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Makatibu wakuu wawili wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana wamemwandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu katika chama hicho, Pius Msekwa wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi na uongo.

Lakini spika huyo wa zamani wa Bunge amewajibu, akiwashauri “wajibu mapigo”.

Mwenyekiti wa baraza hilo ni Rais Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili.

Makamba na Kinana, ambao walishika nafasi hizo kwa kufuatana wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, wamesema wametuma malalamiko yao “kwa kuzingatia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122”.

“Tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kulishughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya chama na nchini,” wanasema katika barua yao.

Makamba alikuwa katibu mkuu wa sita na Kinana (wa nane) wametoa taarifa ya maandishi kwa umma Julai 14, 2019 ambayo wameisaini wakimlalamikia mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Advertisement

“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo,” inasema taarifa hiyo.

Wastaafu hao wanasema wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu taarifa wanazodai za uzushi kwa nyakati mbili tofauti.

Walisema kwa sasa Watanzania wanajua kuwa yanayosemwa na mtu huyo si ya kwake.

Wanasema mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo, ambaye amemtaja lakini jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, anatumwa na nani?

Advertisement