VIDEO: Nyerere ni nani? Vijana Vs Wazee

Muktasari:

Jina la Julius Nyerere linaendelea kusikika kutokana na kutumiwa na majengo na maeneo mbalimbali.

Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, ukumbi wa kimataifa wa mikutano na eneo la kupumzikia katikati ya Jiji la Dodoma, yanajulikana kwa jina la Julius Nyerere.

Dar/ mikoani. Jina la Julius Nyerere linaendelea kusikika kutokana na kutumiwa na majengo na maeneo mbalimbali.

Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, ukumbi wa kimataifa wa mikutano na eneo la kupumzikia katikati ya Jiji la Dodoma, yanajulikana kwa jina la Julius Nyerere.

Gazeti la Mwananchi liliongea na vijana 70 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 22 kujua wanalifahamu vipi jina hilo, na wengi wameonyesha kutomjua hasa muasisi huyo wa Taifa zaidi ya kumsikia katika simulizi za watu wazima na kumsoma katika mitandao ya kijamii.

Walikuwa wakijibu swali la Mwananchi kuhusu jinsi wanavyomfahamu rais huyo aliyeongoza nchi kwa miaka 23.

Nyerere aliongoza harakati za uhuru zilizofanikiwa mwaka 1961 na alifariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza alikokuwa katika matibabu, ikiwa ni miaka 14 tangu alipong’atuka madarakani kuachia wengine kuongoza nchi.

Kati ya vijana 70 waliohojiwa, 51 wanamfahamu kwa simulizi, kumi kwa kusoma vitabu vyake au vinavyomzungumzia aliyoyafanya na tisa wamemsoma shuleni.

“Tunamkumbuka Mwalimu kupitia kwa wazee mbalimbali wakimsimulia kupitia kwenye vijiwe vya kahawa na kucheza bao,” alisema Juma Athanas mwenye umri wa miaka 22 ambaye ni mkazi wa Sengerema.

“Na sisi tukajua kuwa kama asingekuwa Mwalimu Nyerere, wakoloni wangeendelea kutawala Taifa letu.”

Kijana mwingine mwenye umri wa miaka 22, Obadia Anthony alisema anamfahamu Nyerere kutokana na kusoma historia.

“Ninamfahamu Mwalimu Nyerere kutokana na kusoma historia yake na kuelezwa na walimu shuleni,” alisema Anthony.

“Mwalimu Nyerere ndiye Rais wa kwanza wa Tanganyika na historia yake inamtaja kuwa alikuwa mtu mzalendo”

Vijana wengi waliohojiwa na Mwananchi walionekana kumfahamu kutokana na kusoma historia kuwa ndiye aliyeongoza mapambano ya kudai uhuru, lakini hawaonekani kama wanafahamu kuendelea kuishi kwa falsafa zake katika maisha ya sasa.

“Namfahamu Mwalimu Nyerere kama Baba wa Taifa na Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanzania,” alisema George Kariuki, mkazi wa Moshi.

“Katika historia (Nyerere) anatajwa kama mmoja wa viongozi waliopinga nchi kutawaliwa na wakoloni na aliipatia Tanganyika Uhuru 1961.”

Pengine ni kutokana na hali hiyo, watu wenye umri mkubwa zaidi waliozungumza na Mwananchi wanashauri wameshauri njia bora za vijana kujua yaliyofanywa na Rais huyo wa Awamu ya Kwanza.

Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa alisema vijana wengi hawamfahamu Mwalimu Nyerere hivyo jitihada zinapaswa kufanyika ili wamjue.

Mwanadiplomasia mkongwe, Balozi Juma Mwapachu alisema: “Vijana wengi wa rika la sasa hawamfahamu Mwalimu (Nyerere) na hakuna wito wa kutaka watu kuandika jinsi walivyomfahamu Mwalimu ili vijana waweze kujifunza.”

Ni kutokana na hali hiyo, kuanzia kesho gazeti la Mwananchi litaanza kukuletea mfululizo wa makala zinazozungumzia maisha ya Mwalimu Nyerere kielimu na kikazi, harakati za uhuru, falsafa na changamoto alizokumbana nazo kabla ya kifo chake.