VIDEO: Watuhumiwa uhujumu uchumi 467 waandika barua, Magufuli aongeza siku saba

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amewasilisha taarifa ya watuhumiwa wa uhujumu uchumi walioomba kukiri makosa na kurudisha fedha.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amesema watuhumiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi wameandika barua za kuomba kukiri makosa na kurudisha fedha Sh107.84 bilioni.

Akiwasilisha taarifa yake leo Jumatatu Septemba 30, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Mganga amesema watuhumiwa wameitikia wito alioutoa Rais John Magufuli

“Watu wameitikia ushauri wako (Rais Magufuli) na tumeufanyia kazi ushauri wako kwamba kwa ndani ya siku saba ambazo ziliishia Jumamosi ya Septemba 28, 2019.”

“Katika kipindi hiki, ofisi yangu imepokea barua za washitakiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi walioomba kukiri makosa yao na kurejesha fedha walizowaibia Watanzania,” amesema Mganga

Ameendelea kusema, “Barua hizi zimeendelea kuja Jumamosi na mpaka jana niliona zinakuja kwa kuwa zilichelewa kutoka mikoani kuja ofisini.”

DPP amemuomba Rais Magufuli kuongeza siku tatu kwaajili ya kuwapa nafasi watuhumiwa wa uhujumu uchumi walio tayari kutubu na kurejesha fedha na mali ambao barua zao zimechelewa kufika ofisini kwake.

Akijibu ombi hilo, Rais Magufuli ametoa siku saba kuanzia leo Jumatatu Septemba 30, 2019 hadi Oktoba 6, 2019.

“Nimetoa siku saba hizi na baada ya hizi sitatoa tena,” amesema Rais Magufuli

Rais Magufuli amemuomba DPP, Mganga kuharakisha uchambuzi kwa watuhumiwa 467 waliomuandikia barua ili watuhumiwa hao wawe huru na kwenda kushirikiana na familia zao.

Septemba 22, 2019 Rais Magufuli alipokuwa akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, alitangaza siku saba kwa watuhumiwa wa mashtaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambao watakuwa tayari kukiri makosa na kulipa fedha wanazodaiwa kuachiwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi