Vigogo wabwagwa Uchaguzi Mkuu wa 1975

Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 26, 1975, zaidi ya asilimia 75 ya wabunge walioshinda mwaka 1970, walijikuta wakipigwa mweleka.

Miongoni mwa wabunge waliobwagwa katika uchaguzi huo ni mawaziri watatu; Simon Chiwanga aliyekuwa Waziri wa Elimu, Musobi Musobi Mageni (Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini) na Saleh Tambwe (waziri mdogo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki).

Chiwanga, ambaye pia ni padri wa Kanisa Katoliki, aligombea kiti cha Dodoma Mjini ambako akipigwa mweleka na padri mwenzake, Severino Supa aliyepata kura 24,865. Padri Chiwanga alipata kura 20,507.

Huo ulikuwa ni uchaguzi wenye ushindani mkali kuwahi kutokea katika jimbo hilo. Ushindani huo ulitokana na ukweli kwamba wagombea wote walikuwa mapadri wa Kanisa Katoliki, pili wote walikuwa wasomi na tatu wote walikuwa wabunge.

Awali Padri Supa, ambaye alikuwa na Ph.D, alikuwa mbunge wa taifa akiwakilisha Jumuiya ya Wazazi (TAPA).

Mageni, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini, aligombea jimbo la Kwimba alikopata kura 16,461, alishindwa na Chimani Masanja aliyepata kura 44,944.

Itakumbukwa katika Uchaguzi Mkuu wa 1965, Mageni aligombea jimbo la la Kwimba Kusini na kushinda. Aligombea tena katika uchaguzi uliofuata wa mwaka 1970 katika jimbo la Mwamashimba. Nako alishinda. Lakini akashindwa katika uchaguzi wa mwaka 1975.

Mageni ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Kinamweli wilayani Kwimba, aliteuliwa na Mwalimu Nyerere Alhamisi ya Februari 17, 1972 kuwa waziri. Baada ya kupoteza jimbo lake la uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa 1975, mwaka 1978 Mwalimu Nyerere alimteua tena kuwa mkuu wa Wilaya ya Chunya.

Mawaziri walioshinda ni pamoja na John Malecela (Mambo ya Nje), Mrisho Sarakikya (Utamaduni wa Taifa na Vijana), Patrick Qorro (waziri mdogo, Ofisi ya Waziri Mkuu), Osiah Mbembela (Waziri wa Elimu), Mussa Massomo (waziri mdogo, Ofisi ya Waziri Mkuu).

Malecela, aliyegombea Dodoma Vijijini, alipata kura 67,591 na kumshinda Bernadini Mwanja aliyepata kura 10,844..

Sarakikya aligombea jimbo la Arumeru na kupata kura 36,124 dhidi ya kura 25,093 za Obed Simeon Ole Mejooli, wakati Patrick Qorro alishinda Jimbo la Mbulu kwa kura 40,769 dhidi ya Geay Damian Buha aliyepata kura 11,297.

Katika Jimbo la Ileje, Mbembela alishinda Stephen Kibona kwa kupata kura 9,271 dhidi ya 5,239 za mpinzani wake.

Pia Waziri Massomo alipata kura 41,205 na hivyo kumbwaga Chomba Joseph Nyosole aliyepata kura 1,962.

Mgonja atetea ubunge

Wengine walioshinda ni Spika wa Bunge, Chifu Erasto Mang’enya na katibu wa TANU wa mkoa wa Mtwara, Chediel Mgonja.

Mgonja ni mtu mwingine maarufu katika uchaguzi huo. Mgonja ni miongoni mwa Watanzania sita waliotunukiwa tuzo kwa kushiriki katika shindano la kutunga wimbo wa Taifa mwaka 1981.

Alienda kusoma masomo ya diplomasia mwaka huo katika Chuo Kikuu cha Cambrige na aliporudi mwaka 1962, alipelekwa ubalozini jijini New York, lakini mwaka 1964 aliomba kurejea nyumbani kwa ajili ya kugombea ubunge wa Pare, ambako alimshinda aliyekuwa waziri mdogo na katibu mwenezi wa Tanu, Elias Kisenge.

Pia anajulikana kwa kuwa mmoja wa wabunge waliojitolea kwenda katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uwaziri na mwaka 1977, akiwa Waziri wa Utamaduni na Michezo, alikataa shinikizo la Marekani la kususia Michezo ya Olimpiki ya Moscow, licha ya taifa hilo kumtuma balozi wake, Muhamed Ali, aliyekuwa bingwa wa ngumi za uzito wa juu duniani, kufanya ushawishi huo.

Mshindi mwingine maarufu katika uchaguzi huo alikuwa Jackson Makweta, aliyegombea Jimbo la Jimbo la Njombe na kumshinda Levi Masoke kwa kupata kura 55,182 dhidi ya 23,041 za Masoke.

Makweta aliweka rekodi ya kuwa waziri kwa kipindi cha miaka 25 kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 2010, na akiwa Waziri wa Elimu, mwaka 1982, aliiongoza “Tume ya Makweta” iliyoteuliwa na Rais kuangalia uboreshaji wa mfumo wa elimu na mitaala, ilitoa mapendekezo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutaka Kiswahili kitumike kufundishia kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu.

Lakini ilichukua muda mrefu kutekeleza mapendekezo hayo kutokana na uchumi kuyumba duniani na kuiathiri Tanzania.

Pia aliwahi kuwa waziri wa maji nishati na madini katika awamu ya pili. Makweta alifariki Novemba 17, 2012 na jimbo hilo kwa sasa linashikw ana Deo Sanga.

Pia Edgar Maokola-Majogo, ambaye baadaye alikuja kushika uwaziri, aliibuka shujaa katika uchaguzi wa mwaka huo. Majogo alipata kura 18,697 na kumshinda mpinzani wake, Marcus Felix Millanzi aliyepata kura 12,101.

Katika hafla moja iliyofanyika mwaka 2012, Majogo aliwashauri wanasiasa wanaopata nafasi kubwa kama za uwaziri, kuwa makini na watu wanaowazunguka kwa kuwa baadhi ni “marafiki na wengine ni wanafiki”.

Alisema baada ya kupoteza uwaziri, nusu ya marafiki walimkimbia.

“Walipogundua sina cheo, tena serikalini walinikimbia mmojammoja,” alisema Majogo.

“Nawaasa viongozi wa serikali, mkiwa madarakani huku mkitembelea magari yenye bendera za taifa, mtazungukwa na marafiki lakini baadhi yao ni wanafiki.”

Alisema wengi wataonyesha unyenyekevu, lakini baada ya kustaafu watashangaa hawaonekani.

Katika uchaguzi huo, Chrisant Mzindakaya pia aling’ara baada ya kushinda kwa tofauti ya takriban nusu ya kura zote katika jimbo la Sumbawanga Vijijini. Alipata kura 40,341 dhidi ya Mfupe Pangani aliyepata kura 22,735.

Dk Mzindakaya, mmoja wa wabunge waliokaa kwa muda mrefu, aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1965 akitokea Jimbo la Ufipa Kusini, lakini mbio zake ziliingia doa mwaka 1981 baada ya ushindi wake kutenguliwa mahakamani kwa hoja kwamba alikiuka taratibu.

Hiyo haikumzuia kukaa nje ya chombo hicho cha kutunga sheria. Mwaka 1982 aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya na hivyo kurejea bungeni kwa tiketi hiyo.

Alijipatia umaarufu kwa kulipua mabomu bungeni wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Alianza na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba, kutokana na kashfa ya sukari iliyosababisha waziri huyo kujiuzulu na baadaye kumlipua Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi ambaye pia alijiuzulu na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga.

Kibao kilimgeuka alipolipuliwa akidaiwa kukopeshwa fedha kwa ajili ya kujengea kiwanda cha kusindika nyama mkoani Rukwa na kudhaminiwa na Serikali lakini hakurudisha mkopo.

Katika Jimbo la Lushoto alishinda Amiri Hoza kwa kura 39,152 dhidi ya kura 25,908 za mpinzani wake, Joseph Mandia.

Katika Jimbo la Biharamulo, mshindi alikuwa Stanslaus Kasusura aliyepata kura 25,894 dhidi ya mpinzani wake, John Kabengo aliyepata kura 11,929.

Katika toleo lijalo tutaangazia namna Rais mteule alivyoapishwa na kuunda Baraza la Mawaziri.