Vijiji 8,587 Tanzania vimesambaziwa umeme wa Rea – Waziri Kalemani

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani

Muktasari:

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunganishia wananchi umeme vijijini ili kuwawezesha wale waishio katika maeneo hayo kujiingizia kipato kwa kufanya biashara mbalimbali.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunganishia wananchi umeme vijijini ili kuwawezesha wale waishio katika maeneo hayo kujiingizia kipato kwa kufanya biashara mbalimbali.

Dk Kalemani ameyasema hayo leo Jumapili Februari 2, 2020 alipokuwa akitoa utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne.

Akitoa taarifa hiyo Kalemani amesema katika Mradi wa usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) jumla ya vijiji 8,587 kati ya vijiji 12,268 vimepelekewa umeme.

 Amesema kuwa awali mwaka 2014 vijiji 562 pekee vilikuwa na umeme na mwaka 2015 viliongezeka hadi kufikia 2018.

”Tumepiga hatua, ukiangalia hali ilivyokuwa mwaka 2014, 2015 na sasa ni tofauti, wananchi katika maeneo mengi ya vijijini wamepata umeme na tupo kwenye mchakato wa kumalizia vijiji vilivyobaki, tunataka hadi kufikia Juni 2021 vijiji vyote viwe vimesambaziwa umeme,” amesema Dk Kalemani.

Ameongeza kuwa lengo la kupeleka umeme vijijini ni kuvihamisha viwanda ambavyo vilitakiwa mijini na kwenda  vijijini ili kufuata malighafi zinapotoka.

”Huwezi kujenga viwanda vya kuchakata  pamba mijini wakati pamba inalimwa vijijini na hii itasaidia vijana wengi kupata ajira na kuacha tabia ya  kutoka vijijini kuja mjini kwa sababu wanaweza kutumia umeme wakiwa vijijini kwa ajili ya kufanya shughuli zao,”.

Amesema kwa sasa hali ya upatikanaji wa umeme inaendelea kuimarika, na kuwatoa hofu wananchi kuwa Serikali itaendeleza kuhakikisha umeme unapatikana wa kutosha kwa ajili ya kurahisisha uzalishaji.

“Mwaka 2015 tulikuwa na Megawat 1038 na sasa tuna Megawat 1602 kwa hiyo tumeongeza Megawat 480 mpya na maeneo yaliyoongeza megawat ni miradi ya kuzalisha na kufua umeme kwa rasilimali ya gesi iliyopo Kinyerezi,” amesema.