Shamte wa Katani na wenzake waswekwa ndani tuhuma za Sh54bn

Tanga. Kikao cha kupokea ripoti ya mkaguzi mwandamizi wa ndani wa Wizara ya Fedha kuhusu mgogoro wa wakulima wadogo wa mkonge na kampuni ya Katani Limited, kimegeuka mwiba kwa viongozi wa ngazi za juu wa kampuni hiyo baada ya kutolewa amri kuwa wakamatwe.

Miongoni mwa viongozi hao yumo mkurugenzi mtendaji mstaafu wa kampuni hiyo, Salum Shamte. Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela aliamuru kukamatwa kwao kutokana na tuhuma za kuhusika na upotevu wa zaidi ya Sh54 bilioni zikiwamo fedha za Serikali.

Wengine waliokamatwa ni Juma Shamte ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa sasa wa Katani Limited, Fadhili Malima (mkurugenzi wa fedha), Theodora Mtejeta (ofisa uhusiano) na mjumbe wa bodi, Fatma Diwani.

Sambamba na polisi, Shigela aliamuru Takukuru kuchunguza tuhuma hizo ili kujulikana ukweli.

Hata hivyo, Shamte alipingana na taarifa hiyo akidai imetengenezwa bila kushirikisha uongozi wa Katani Limited ambao unazo taarifa sahihi kuhusu fedha hizo na matumizi yake.

Akizungumza katika mkutano huo, Shamte alisema Katani Limited ina vielelezo vyote kuhusiana na mgogoro na kwamba ripoti hiyo ipitiwe upya ili kupatikana ukweli.

“Ripoti hii imeandaliwa kwa lengo la kutupaka matope na kutuharibia hadhi na heshima yetu tuliyolitumikia taifa letu kwa uzalendo wa hali ya juu, hakuna fedha yoyote iliyoptea kwa sababu Katani hesabu zake ziko wazi,” alisema.

Mkaguzi wa ndani mwaandamizi wa Wizara ya Fedha, Idrisa Ally alieleza kuwa ukaguzi huo ulianza Januari 22 hadi Februari 22 ukianzia mwaka 2008 hadi 2018.

Alisema ukaguzi huo ulilenga kuangalia miamala ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakulima na fedha za Saccos ya wakulima hao na mikataba iliyoingiwa baina ya pande hizo tatu.

Alieleza kuwa katika ukaguzi huo, zaidi ya Sh54 bilioni hazikufahamika zilipo au matumizi yake yakiwamo madeni ya wakulima, makato ya NSSF,mkopo na kutolipwa kwa kodi ya Serikali.