Vitambulisho vinavyokubaliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa hivi hapa

Saturday August 24 2019

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma . Kanuni za uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mtaa za mwaka 2019 nchini Tanzania zimeainisha aina nane za vitambulisho ambavyo msimamizi wa kituo cha uchaguzi anaweza kumtaka mpiga kura aonyeshe ili kujiridhisha na jina kama ndilo liko katika orodha ya mpiga kura.

Kanuni hizo zimetolewa jana Ijumaa Agosti 23 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo jijini Dodoma mbele ya viongozi mbalimbali wa mikoa na wadau wa siasa.

Kanuni hizo zimetaja vitambulisho hivyo ni kitambulisho cha mpiga kura, cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya bima ya afya, cha shule au chuo, cha mfuko wa hifadhi ya jamii, leseni ya udereva na kitambulisho cha Taifa.

Kanuni hiyo ya 33 kifungu cha pili kinasema, "Msimamizi wa kituo anaweza kumtaka mpiga kura aonyeshe kitambulisho kitakachoonesha kuwa jina la mpiga kura huyo ndio lililomo kwenye orodha ya wapiga kura."

Advertisement