VIDEO: Vyakula havishikiki ujenzi wa daraja ukiendelea

Muktasari:

Wakati ujenzi wa daraja la Kiyegeya barabara ya Morogoro- Dodoma ukiendelea baada ya kuzolewa na maji, baadhi ya abiria na madereva waliokwama kuendelea na safari wamesema wanauziwa chakula kwa bei ya juu kuliko awali.

Morogoro. Wakati ujenzi wa daraja la Kiyegeya barabara ya Morogoro- Dodoma ukiendelea baada ya kuzolewa na maji, baadhi ya abiria na madereva waliokwama kuendelea na safari wamesema wanauziwa chakula kwa bei ya juu kuliko awali.

Daraja hilo lililopo Gairo linalounganisha mikoa ya Dodoma na Morogoro lilisombwa na maji juzi Jumatatu Machi 2, 2020 saa 9 alasiri kufuatia mvua zinazoendelea.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Machi 4, 2020 kwa nyakati tofauti,  Mohamed Idda anayeelekea  Wilaya Mpwapwa mkoani Dodoma amesema alipanda basi jana huku abiria wakiahidiwa kuwa wakifika eneo hilo watahamishiwa katika usafiri mwingine, ahadi ambayo imeota mbawa.

Amesema kwa sasa sahani  moja ya chakula inauzwa Sh3,500  hadi 4,500 badala ya Sh2,000, “vinywaji sasa ni Sh1,000 hadi 1,500 kutoka Sh500 hadi Sh700.”

Naye Jonas Mdabi  amesema katika eneo hilo shida ni huduma ya choo na eneo la kuoga.

Utingo wa lori, Hamza Gidion amesema kwa siku tatu wamekuwa mkoani Morogoro wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa daraja, “hatuwezi kupita Iringa kwa kuwa hatuna mafuta ya kutosha kupita huko.”

Mwananchi limeshuhudia msururu wa magari katika eneo hilo huku mamia ya watu wakihaha huku na kule kutafuta mahitaji mbalimbali.

Jana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema hadi usiku wa kuamka leo magari yatakuwa yanapita eneo hilo jambo ambalo limekuwa tofauti.