Waandamana London kuunga mkono Maandamano Nigeria

Muktasari:

Karibu watu 500 leo Jumamosi wameandamana katika mitaa ya London kuunga mkono maandamano ya vijana nchini Nigeria ambayo yamesababisha taifa zima kuwa katika wasiwasi.

London, Uingereza (AFP). Karibu watu 500 leo Jumamosi wameandamana katika mitaa ya London kuunga mkono maandamano ya vijana nchini Nigeria ambayo yamesababisha taifa zima kuwa katika wasiwasi.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ndiye anayelengwa na hasira za watu kutokana na jinsi anavyoshughulikia maandamano ya kupinga ukatili wa polisi na vitendo vya Kikosi cha Kukabili Ujambazi, maarufu kwa jina la Sars.

Waandamanaji, wengi wakiwa Wanigheria waliolowea Uingereza, walishika mabango yaliyoandikwa End Sars au ondoa kikosi cha kukabili ujambazi, na mengine kuandikwa "komesha ukatili wa polisi" huku wakiimba "Buhari ni mtu mfu" wakati wakitembea katika mitaa ya mji huo mkuu wa Uingereza.

Wengine walikuwa wakipunga bendera za Nigeria, huku baadhi wakiwa wameimwagia rangi nyekundu ionekane kama damu, na wengine kuvalia barakoa za kijani na nyeupe wakati wakipita katika maeneo muhimu ya London, yakiwemo bustani ya Bunge na ofisi za BBC.

Buhari amekifuta kitengo hicho kinachoogopwa cha polisi na kuahidi kufanya mageuzi, lakini vijana wanataka mabadiliko zaidi.

Kitendo cha polisi kufyatulia risasi waandamanaji ambao hawakuwa na silaha kilisababisha dunia nzima ilaani na kuibua vurugu katika jiji hilo kubwa kuliko yote barani Afrika.