Waandishi wa habari wa kimataifa kushiriki onyesho la utalii Tanzania

Mkurugenzi mwendeshaji wa TTB, Devota Mdachi

Muktasari:

Wakala wa kampuni za utalii na waandishi wa habari wa kimataifa zaidi ya 400 wanatarajiwa kushiriki onyesho la kimataifa la utalii litakalofanyika Tanzania kuanzia Oktoba 18 hadi 20, 2019.

Dar es Salaam. Wakala wa kampuni za utalii na waandishi wa habari wa kimataifa zaidi ya 400 wanatarajiwa kushiriki onyesho la kimataifa la utalii litakalofanyika Tanzania kuanzia Oktoba 18 hadi 20, 2019.

Onyesho hilo la Swahili International Tourism Expo (S! TE) limeandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara wadogo wa utalii wa Tanzania  na wafanyabiashara kutoka masoko makuu ya utalii duniani.

Mkurugenzi mwendeshaji wa TTB, Devota Mdachi amesema  kampuni 200 za waonyeshaji kutoka nchi 60 zitashiriki kwenye onesho hilo.

Amesema bodi hiyo imepokea uthibitisho kutoka ofisi za balozi za Tanzania kuwa zimewafanyia usahili  washiriki kutoka nchi 23 duniani.

Amesema pamoja na maonyesho ya huduma za utalii, kutakuwa na semina, mada mbalimbali zitawasilishwa na watalaam waliobeba kwenye sekta hiyo.

“Sambamba na hayo yote kutakuwa na vyakula vya asili ya Kitanzania, maonesho ya mitindo ya mavazi, michezo ya jukwaani na mapishi,” amesema.

Mdachi amesema baada ya kumalizika kwa maonesho,  Oktoba 21, 2019 wameandaa ziara ya mawakala wa utalii na waandishi wa habari wa kimataifa kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii.

Maeneo yatakayotembelewa ni Hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro, mlima Kilimanjaro, fukwe za Tanga, mapango ya Amboni, msitu wa Magoroto, Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Zanzibar na Mafia.