Breaking News

Waathirika wa mafuriko Dar waomba msaada

Sunday October 18 2020

 

By Fortune Francis, Mwananchi

Dar es Salaam. Siku chache baada ya mvua iliyonyesha kwa siku mbili jijini hapa na kuathiri baadhi ya miundiombinu, wakazi waishio mabondeni wameiomba Serikali kuwasaidia vitu mbalimbali ikiwemo chakula, magodoro na vifaa vya wanafunzi.

Mvua hiyo iliyonyesha Oktoba 14 na 15 ilisababisha barabara kutopitika kutokana na nyingi kufungwa baada ya madaraja kufurika huku baadhi ya watu wakifika majumbani kwao usiku wa manane na wengine alfajiri.

Mwananchi ilifika jana katika maeneo mbalimbali ikiwamo Jangwani na Kigogo na kushuhudi baadhi ya familia zikilala kwenye mikeka na wengine wakiendelea kutoa maji na tope lililokwama ndani ya nyumba zao.

Mkazi wa Msimbazi, Mwanabibi Nassibu alisema mvua iliyonyesha ilisababisha vifaa mbalimbali kusombwa na maji, kukosa chakula na sehemu ya kulala.

“Hapa unapoona ndio tunaanza kutoa maji ndani, hatuna chakula wala sehemu ya kulala watoto, madaftari ya watoto yamesombwa na maji,” alisema Mwabibi.

Alisema baada ya mvua ile walikusanywa katika Shule ya Sekondari Msimbazi kwa ajili ya kupewa chakula lakini kazi hiyo haikufanyika hivyo wanaomba Serikali iwasaidie.

Advertisement

Martha Anthon, mkazi wa Kigogo alisema wamekuwa kama watoto yatima kila wakati wa mvua na wameiomba Serikali iwaboreshee miundombinu kabla ya mvua hazijaanza kwa nyingi.

Alisema kwa sasa hawana kitu chchote kwa kuwa vitu vyote viliondoka na mji ikiwamo magodoro, chakula na nguo.

“Kama mnavyotuona tunalala chini, hatuna vitanda watoto shule hawajaenda shule na hata walioenda walisoma madaftari ya wenzao,” alisema Martha.

Mkazi wa Jangwani aliyejitambulisha kwa jina moja la Husna, alisema kunapotokea maafa kama hayo wapo watu wanaopita wakiandikisha majina lakini hakuna msaada wowote wanaopelekewa.

Alisema wamekuwa wakifika watu kwa ajili ya kujua tu matatizo yao hakuna msaada na baada ya mvua wamekuwa wakipewa kauli za kejeli wakiambiwa wahame maeneo hayo sio ya kuishi.

“Kila wakati wa mvua maneno ni haya haya lakini hatupati msaada wowote jana walikuja watu hatujaona msaada ila na sisi pia ni binadamu kama wao,” alisema Husna huku akimtaka mwandishi kuondoka eneo hilo.

Advertisement