Wabunge Eala wavutana kumchagua mwenyekiti wa muda

Muktasari:

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) leo Jumatatu Februari 24, 2020 wamevutana kuhusu kanuni wakati wa uchaguzi wa mwenyekiti wa kuongoza kikao cha Bunge hilo linaloendelea na vikao vyake mjini Arusha.

Arusha. Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) leo Jumatatu Februari 24, 2020 wamevutana kuhusu kanuni wakati wa uchaguzi wa mwenyekiti wa kuongoza kikao cha Bunge hilo linaloendelea na vikao vyake mjini Arusha.

Hali hiyo imejitokeza kutokana na Spika wa Bunge hilo, Martin Ngoga  kupata udhuru.

Kwa mujibu wa mkataba wa ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ibara ya 56 pamoja na kanuni za Bunge zinatoa nafasi ya kuchaguliwa mwenyekiti  wa muda katika kipindi ambacho Spika atakua hayupo.

Katibu wa Bunge hilo, Charles Kadonya  amesema tukio kama hilo limewahi kufanyika wakati wa Bunge la kwanza na mbunge kutoka Tanzania, Mabere Marando alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa muda katika kipindi ambacho hakuwepo Spika.

Baada ya ufafanuzi huo, wabunge walimpendekeza Leontine Nzeyimana  wa Burundi ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Afrika Mashariki pamoja na  Fatuma Ndagiza wa Rwanda aliyewahi kuwa balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania.

Katika kuendeleza hali ya mshikamano na upendo miongoni mwao, Mbunge kutoka Tanzania, Dk Abdullah Makame alipendekeza kusitisha kwa muda ibara ya nne inayotaka kura zipigwe kwa kuinua mikono akidai jambo hilo lingeondoa umoja wao .

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge na Mbunge wa Kenya ,Aden Abdukadir alipendekeza hoja kupelekwa kwa wakuu wa nchi za EAC ili Bunge hilo liwe na naibu Spika atakayekuwa akiendesha shughuli za Bunge kama Spika hatokuwepo.

“Hili ni jambo muhimu sana kuhakikisha tunapeleka hoja ya kuwa na naibu Spika suala hili litatupa nafasi ya kuhakikisha shughuli za Bunge hazikwami. Spika ni binadamu kama sisi ambaye kwa namna moja au nyingine anaweza kupata dharura,” amesema Aden

Katika uchaguzi huo, Fatuma alipata kura 18 huku Nzeyimana akipata kura 27  na kuongoza kikao cha Bunge.