Wachumi Tanzania walivyomzungumzia msomi UDSM aliyefariki dunia

Wednesday January 08 2020

Dar es salaam. Nyuso za majonzi, huzuni zimetawala leo Jumatano Januari 8, 2020 wakati msomi nguli wa uchumi Tanzania, Profesa Amon Mbelle (66) alipofunga safari ya mwisho duniani katika makaburi ya Kondo jijini Dar es salaam.

Mshauri huyo wa uchumi katika vipindi tofauti vya uongozi wa Serikali ya Tanzania,  alikutwa amefariki dunia Januari 4, 2020 nyumbani kwake mtaa wa Nyanza, Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, haikufahamika mapema chanzo cha kifo chake.

Kabla ya umauti wake, Profesa Mbelle alikuwa mwanataaluma katika Idara ya uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa miaka 38, akifanya tafiti za uchumi, machapisho pamoja na kuandika vitabu.

Mamia ya watu mbalimbali leo Januari wamejitokeza nyumbani na baadaye kuaga mwili wake katika kanisa Katoliki lililopo Kunduchi Mtongani.

Ilikuwa ni hali ya majonzi hususani kwa wanafamilia huku nyimbo za maombolezo zikitawala nyumbani. Idadi ya watu na msongamano wa magari ulikuwa mkubwa.

Advertisement

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga pamoja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya hawakuwa tayari hata kuzungumzia tukio hilo.

"Ni mshtuko mkubwa sana kwa kweli, ni maumivu makali. Kama Idara ya uchumi (UDSM) tutaangalia namna ya kumuenzi hata kuandika kitabu kuhusu maisha yake, " amesema Profesa Haji Semboja aliyekuwa Idara moja na marehemu.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Repoa, Dk Donald Mmari amesema licha ya kumpoteza mwalimu aliyemfundisha chuoni hapo  pia amepoteza kiungo muhimu waliyeshiriki pamoja uandaaji wa mkukuta awamu zote mbili.

"Hata mpango wa Maendeleo ya Taifa unaotumika katika awamu hii ya tano alihusika kuandaa kwa hiyo unapozungumzia maendeleo ya kiuchumi Tanzania lazima tukumbuke nafasi yake, "alisema Dk Mmari.

Aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango, Dk Servacius Likwelile amesema marehemu alihusika katika timu ya uandaaji wa mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini katika awamu ya kwanza na Ile ya pili.

Mkukuta awamu ya kwanza ilianza 2005 na awamu ya pili 2010. Kwa mujibu wa tovuti ya serikali, tangu 2005 uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia saba, kuendana na lengo lililowekwa la asilimia sita hadi nane kwa mwaka.

"Mie nimefanya naye kazi UDSM, mapendekezo ya utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Millennium (SDGs) alihusika pia katika ufanikishaji wake kwa hiyo ni Pigo kubwa kupoteza nguzo muhimu sana," amesema Dk Likwelile.

Mwakilishi wa Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi (ESRF), Dk Oswald Mashindano amesema marehemu alikuwa mmoja wa watafiti kwa takribani miaka 20 katika taasisi hiyo.

"Alikuwa nguzo na tegemeo kubwa sana, tafiti zake zilikuwa msaada na matokeo chanya katika jamii," amesema Dk Mashindano.

Advertisement