Wafanyabiashara Dodoma watakiwa kuchangamkia mikopo

Muktasari:

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi ametoa wito kwa wafanyabiashara mjini humo kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.

Dodoma. Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi ametoa wito kwa wafanyabiashara mjini humo kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.

Amesema kwa kufanya hivyo watanufaika na ongezeko kubwa la fursa za kibiashara zinazoibuka  katika Jiji hilo ambalo ni makao makuu ya nchi.

Akizungumza katika uzinduzi wa klabu ya wafanyabiashara ya Benki ya NBC Mkoa wa Dodoma jana jioni Septemba 11, 2019, Kunambi mbali na kuipongeza benki hiyo kwa mabadiliko makubwa ya huduma, amesema bado ipo haja kwa wafanyabiashara kuitumia vyema kupata nguvu ya kiuchumi itakayowawezesha kufaidi fursa ya mabadiliko ya ukuaji wa uchumi.

“Dodoma kwa sasa kuna utekelezaji wa miradi mikubwa mingi ikiwemo barabara, stendi ya mabasi ambayo ni kubwa zaidi Afrika Mashariki, upanuzi wa uwanja wa ndege, ujenzi wa viwanja vya mapumziko ambayo vitachochea mzunguko mkubwa wa pesa na ongezeko la watu.”

“Ni fursa kwa wafanyabiashara kushirikiana vyema na benki kama NBC ili kukuza mitaji itakayowawezesha kufanya uwekezaji utakaowanufaisha na mabadiliko hayo,’’ amesema Kunambi aliyehudhuria hafla hiyo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa huo, Dk Bilinith Mahenge.

Ametoa mfano umuhimu wa wafanyabiashara kuwekeza kwenye sekta ya usafiri ambayo kwa sasa Serikali ipo kwenye mpango wa kuondoa gari dogo za abiria maarufu kama vipanya kwenye mizunguko ya mjini  ili kutoa fursa kwa magari makubwa kufanya kazi hiyo.

Akizungumza kuhusu uanzishwaji wa klabu hiyo, mkuu wa kitengo cha wateja wa kati na wadogo wa benki ya NBC, Evance Luhimbo amesema pamoja na mambo mengine, klabu hizo zinalenga kutoa mafunzo kwa  wateja wa benki hiyo kuelewa mabadiliko ya uboreshwaji wa huduma za  benki hiyo.

Pia kuwakutanisha pamoja wajadili fursa za kibiashara sambamba na kuwajengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya biashara.