Wafanyabiashara wafunga maduka wakishinikiza mwenzao kulipa kreti la soda

Wednesday October 9 2019

Maduka ya wafanyabiashara kijiji cha Nyamigana

Maduka ya wafanyabiashara kijiji cha Nyamigana kata ya Kagu yakiwa yamefungwa ikiwa ni siku ya nne sasa kwa mgomo wa kudai kret ya soda kutoka kwa mfanyabiashara mwenzao 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected] mwananchi.co.tz

Geita. Wafanyabiashara kijiji cha Nyamigana kata ya Kagu wilayani Geita wamefunga maduka yao na kugoma kuendelea na biashara baada ya mfanyabiashara mgeni aliyehamia kijijini hapo kugoma kutoa kreti moja ya soda kama kiingilio.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho,  Mugwe Sabuni amesema wafanyabiashara hao zaidi ya 20 wamefunga maduka yao kwa siku nne sasa wakishinikiza mfanyabiashara huyo, Frank Lucas kulipa Sh12, 000 ya kreti ya soda kama kiingilio kitakachomwezesha kuendelea na biashara.

Sabuni amesema amefanya jitihada  kutatua mgogoro ili wananchi zaidi ya 300 wa kijiji hicho wapate huduma bila mafanikio baada ya pande zote mbili kuwa na msimamo usiobadilika.

Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo Robart Chale amesema wana utaratibu wao wa kulipia kiingilio kinachojenga umoja.

"sisi tunataka alipe kama halipi aondoke kwenye eneo letu maana huu ni utaratibu wetu akileta kreti ya soda wote tunakunywa" amesema.

Amesema wapo wafanyabiashara 40 na kila mmoja lazima alipe kiingilio kwenye kikundi na ambae hayupo tayari kulipa aondoke kwenye kijiji hicho.

Advertisement

Mfanyabiashara anayetakiwa kulipa Sh12,000,  Frank Lucas amesema hayupo tayari kulipa kiingilio hicho kwa kuwa hakipo kwenye utaratibu wa malipo ya Serikali.

“Nililipa Sh20,000 kama kiingilio cha kijiji na mtendaji alinipa taratibu zote,  kwenye hizi taratibu hakuna kiingilio cha wafanyabiashara," amesema Frank.

Mkazi wa kijiji hicho, Eliakim Kasoga amesema mgomo huo umewaathiri wananchi kwa kuwa hadi maduka ya dawa za binadamu yamefungwa na hawawezi kununua kitu chochote, kulazimika kwenda katika vijiji jirani.

Advertisement