Wafanyabiashara wambana naibu waziri, yeye atumia simu kujiokoa

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,  Abdallah Ulega leo  zaidi ya mara tatu alilazimika kutumia simu yake kiganjani kuwapigia papo hapo baadhi ya watendaji wa taasisi zingine za Serikali ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa mnada wa Pugu, ambao walitaka kujua faida ya ujio wa kiongozi huyo katika eneo hilo.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdallah Ulega ametumia simu yake ya kiganjani kutatua baadhi ya  changamoto zinazowakabili  wafanyabiashara wa mnada wa mifugo wa Pugu.

Tukio hilo, lilitokea leo Alhamisi Januari 2, 2019 wakati wa ziara ya kiongozi huyo katika mnada huo kwa ajili ya kuangalia changamoto zinazoikabili eneo hilo.

Ulega alilazimika kuchukua uamuzi huo, baada ya wafanyabiashara hao kumbana kwa  kutaka kujua ujio wake katika mnada huo una faida gani kwao, kwa maelezo  baadhi ya viongozi wanaokwenda wanashindwa kutatua changamoto zao kikamilifu, licha mnada huo kuingiza fedha nyingi.

Wafanyabiashara hao walimweleza changamoto zinazoikabili eneo hilo ni pamoja uhaba wa maji ya kunyeshwa mifugo, ubovu wa barabara kutoka Gongo la Mboto hadi katika eneo hilo, wafanyabiashara wa nchi za nje kwenda moja kununua mifugo vijijini na ubovu wa eneo la kushusha na kupakia mifugo.

“Mheshimiwa waziri karibu sana hapa mnadani, tumeshuhudia viongozi wengi wakija hapa lakini tukiwaeleza changamoto wanasema wizara yake ndio inahusika. Sasa leo umekuja kama baba je tuna kuuliza ujio wako utakuwa na faida gani kwa wafanyabiashara? amesema Zabron Mahende mmoja wafanyabiashara.

Baada ya maelezo hayo ya Mahende na waliyatoa wenzake, Ulega alitoa simu yake katika mfuko wa koti na kuanzia kumpigia papo hapo mmoja wa manaibu wa wizara ya ujenzi na mawasiliano kuhusu changamoto ya barabara hiyo.

Katika mazungumzo yao, naibu waziri huyo wa ujenzi alimweleza Ulega kuwa barabara hiyo chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini Tarura (Tarura), baada ya maelezo ya kiongozi wa mifugo na uvuvi alimpigia simu mkurugenzi wa Tarura ambaye alikiria suala hilo kulifahamu na kwamba linafanyiwa kazi.

“Hii ndio faida ya ujio wangu baadhi ya mambo mnapata majibu hapa hapa, si mmeona nilivyowapigia simu na majibu waliyoyatoa? Wafanyabiashara waliitikia ndiyo…

“Sasa naombeni muwe watulivu Serikali hii ni moja na mimi nikitoka hapa nitakwenda kuzungumza naye kwa kirefu mkurugenzi huyu kuhusu barabara hii, uzuri wenye lilishaanza kufanyiwa kazi lakini nitakwenda kutilia mkazo,” amesema Ulega.

Awali, kabla ya kuzungumza na wafanyabiashara hao wakati akikagua miundombinu ya mnada huo, Ulega alimpigia simu mmoja wa viongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kanda ya Ukonga, akimtaka kwenda katika eneo na kukutana na viongozi kwa ajili ya kupata suluhisho la maji ya kunyeshwa mifugo.

Ulega alimweleza kiongozi huyo wa Dawasa kuwa maji ya mabwawa yaliyopo katika eneo hilo siyo salama kwa afya ya mifugo, ni vyema wakakutana na viongozi wa mnada na manispaa kwa ajili ya kupanga mpango mkakati wa kukubaliana na hali hiyo.