Wafungwa 293 Dar wanufaika na msamaha wa Rais Magufuli

Waliokuwa wafungwa katika gereza la Ukonga wakiwa wanajiandaa kutoka ndani ya gereza hilo baada ya kupata msamaha wa Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Wafungwa 293 katika magereza za Mkoa wa Dar es Salaam wameachiwa huru leo Jumanne Desemba 10, 2019 ikiwa ni siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kutoa msamaha kwa wafungwa 5,533 nchini.

Dar es Salaam. Wafungwa 293 katika magereza za Mkoa wa Dar es Salaam wameachiwa huru leo Jumanne Desemba 10, 2019 ikiwa ni siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kutoa msamaha kwa wafungwa 5,533 nchini.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa msamaha huo katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika mkoani Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba.

Akizungumza leo Jumanne Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Kambala amesema wafungwa 130 ni wa gereza la Ukonga, 54 gereza la Keko, 74 wa gereza la Segerea na  35 wa Wazo Hill.

Amesema tayari baadhi yao wameanza kuachiwa na wengine wataendelea kutoka kadri taratibu zitakapokuwa zikikamilishwa.

Katibu tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge amesema ameridhishwa jinsi wafungwa hao wanavyoachiwa.

Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amewataka waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi kutothubutu kusaka silaha zao kama walizitelekeza porini.

Baadhi ya wafungwa hao akiwemo Abdallah Said na  Hekima Malandu  wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwasamehe na kuahidi kuwa  watakwenda kuishi vizuri na jamii.