Wagombea 25 CCM wagoma kuchukua fomu uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Wagombea 25 wa ujumbe Serikali ya kijiji na sita wanaowania uenyekiti wa vitongoji kwa tiketi ya CCM wamegoma kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo kwa madai kuwa Halmashauri kuu ya chama hicho Wilaya ya Sengerema imerudisha jina la mgombea asiyekubalika na wananchi.

Buchosa. Wagombea 25 wa ujumbe Serikali ya kijiji na sita wanaowania uenyekiti wa vitongoji kwa tiketi ya CCM wamegoma kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo kwa madai kuwa Halmashauri kuu ya chama hicho Wilaya ya Sengerema imerudisha jina la mgombea asiyekubalika na wananchi.

Wajumbe hao ni wa kijiji cha Kahunda tawi la Kahunda wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza.

Mmoja wajumbe hao, Sikujua Mgaya amelieleza Mwananchi leo  Jumatano Oktoba 30, 2019  kuwa wamegoma kwa kuwa anayewania uenyekiti si chaguo la wananchi.

Hayo yameibuka baada ya jina la Athumani Wambula aliyeshika nafasi ya pili kwenye kura za maoni kuwania uwenyekiti wa kijiji cha Kahunda kupitishwa huku, Masasi Revi aliyeshika nafasi ya kwanza akienguliwa.

“Hatuwezi kuchukua fomu  kugombea nyadhifa zetu huo ndio msimamo wetu na wakitulazimisha kwa namna yoyote tunajiuzulu. Wamrejeshe kipenzi na chaguo la wananchi," amesema Mgaya.

Mkama Tondo, anayewania ujumbe wa nyumba kumi katika kijiji hicho amesema hawapo tayari kutoa ushirikiano wowote wa mgombea huyo, watapinga uamuzi wa chama hicho.

Akizungumzia suala hilo, Wambula amesema ana heshimu uamuzi wa chama chake na kuwaomba wanachama wa chama hicho kumuunga mkono ili aweze kuwatumikia wananchi.

Kwa upande wake, Revi amesema haamini kilichotokea na kubainisha kuwa atakata rufaa, “nitakata rufaa hadi haki itakapotendeka kwa kuwa wanachama walinipatia kura za ushindi na sipo tayari kumuunga mkono mgombea aliyeteuliwa.”

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema,  Marco Makoye amesema wanafuata mapendekezo ya kamati ya siasa ya kata kutokana na sifa za kila mgombea na hupeleka majina hayo Halmashauri kwa kuwa ndio chombo cha mwisho cha kufanya uteuzi wa wagombea.

Kuhusu waliogoma kuchukua fomu amesema hana taarifa ya suala hilo na kuahidi kufuatilia ili kujua ukweli.