MIAKA 20 BILA YA NYERERE: Wahaini wa 1968 walivyoadhibiwa-7

Oscar kambona

Muktasari:

Kama Tanganyika ilikuwa tulivu tangu ilipopata uhuru wake, basi utulivu huo hauna tafsiri ile ile ambayo Watanzania wengi wanaifikiria. Ule mwongo wa kwanza tangu uhuru kulijitokeza mambo mengi, na mengine hayakujulikana sana, na huenda hayatajulikana kamwe. Tukio muhimu zaidi lilitukia mwaka 1968 ambalo baadhi ya maofisa wa serikali walidaiwa kula njama za kuipindua Serikali ya Mwalimu Nyerere. Mwandishi William Shao anaelezea katika makala hii...

Ingawa alikuwa maarufu sana Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla, Mwalimu Julius Nyerere alikabiliana na magumu mengi katika siasa. Alikuwa katika majaribio mengi ya utawala wake kuangushwa. Wengi waliomwinda walikuwa ni wa ndani na nje ya serikali yake. Kulikuwa pia na majaribio mengi ya kuidhoofisha serikali yake.

Nyerere alikabiliana na mataifa ya Magharibi, makaburu wa Afrika Kusini na pia Wareno. Lakini jaribio lililoonekana kuwa kubwa zaidi lilifanywa na Watanzania wenyewe-jaribio la kuipindua serikali yake.

Ingawa kulikuwa na uhaini wa mwaka 1982 kulipokuwa na njama za kuipindua serikali yake ambapo askari 600 walikamatwa na kiasi cha raia 1,000 kutiwa nguvuni Januari 1983 wakidaiwa kushiriki njama za uhaini, hakuna tukio la uhaini lililosikika kama lile la Oktoba 1969.

Ilidaiwa kuwa uhaini huo ulipangwa na Oscar Kambona akishirikiana na maofisa wakubwa wa serikali. Kambona alikuwa ameikimbia nchi tangu Julai 1967, miezi takriban mitano baada ya Azimio la Arusha.

Mashtaka yaliletwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mark Bomani, na baadaye mwanasheria wa Serikali, Nathaniel King.

Pamoja na Oscar Kambona, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Tanganyika, ambaye mwaka 1967 alikimbilia uhamishoni Uingereza mara baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, walihusishwa watu wengine waliodaiwa kula njama za kuiangusha serikali ya Mwalimu Nyerere wakiongozwa na Kambona. Kesi yao ilianza Jumatatu ya Juni 8, 1970 katika Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Mkuu, Philip Telford Georges.

Bila kutambua kilichokuwa kinatokea, watu saba: Gray Likungu Mattaka, John Dunstan Lifa Chipaka, Bibi Titi Mohamed, Michael Marshall Mowbray Kamaliza, Eliyah Dunstan Lifa Chipaka, William Makori Chacha na Alfred Philip Milinga walijikuta wakifikishwa mahakamani kwa kosa la uhaini, wakituhumiwa kula njama za kuiangusha Serikali ya Tanzania na kupanga nyama za kumuua Rais wake, Mwalimu Julius Nyerere.

Gray Likungu Mattaka (34) zamani alikuwa mhariri wa habari wa katika gazeti la chama cha Tanu, The Nationalist na Uhuru. Mattaka alijulikana pia kwa majina mengine ambayo ni Chaima, Kavuma, Mikaya au Edward Kavuma.

John Dunstun Lifa Chipaka (38) alikuwa katibu wa zamani wa chama cha Congress. John Chipaka kwa mujibu wa hati za mashitaka, alikuwa na majina mengine ya bandia kama M. M. Chimwala, Chimwala Ching—wechene, Chimwala au Padre John Chimwala.

Bibi Titi Mohamed (45) ni rais wa zamani wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT). Inasemekana naye alikuwa na majina mengine aliyojiita au kuitwa. Hayo ni pamoja na Mama Mkuu, Mwamba au Anti.

Michael Marshall Mowbray Kamaliza (40) alikuwa Katibu Mkuu wa zamani wa Nuta (Chama cha Wafanyakazi nchini) na kadhalika waziri wa zamani wa kazi na alikuwa na majina mengine ya bandia kama Palijekantu, Bwana Miguu, Wamaliza au Hakuna Kitu.

Eliya Dunstan Chipaka (32) ni ndugu yake John Chipaka. Eliya Chipaka alikuwa ofisa wa zamani katika jeshi. William Makori Chacha (46) alikuwa kanali wa jeshi na majina mengine ya bandia aliyotumia ni pamoja na Ben Tasu au Kitumbo.

Kisha kuna Alfred Philip Milinga (27) aliyekuwa ofisa wa zamani wa jeshi. Oscar Selathie Kambona, alitoroka Tanzania na kwenda kuishi Uingereza.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa kuanzia Jumatatu ya Juni 8, 1970 ilidumu kwa siku 127. Hiyo ilikuwa ni kesi iliyosikilizwa kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Tanganyika na Tanzania kufikia wakati huo. Jaji Georges hakuwahukumu watuhumiwa hao adhabu ya kifo kama sheria iliyokuwa inaelekeza, lakini alimhukumu kila mmoja na hukumu yake.

Bibi Titi Mohamed, Gray Likungu Mataka, Elia Dunstan Lifa Chipaka na John Lifa Chipaka walihukumiwa vifungo vya maisha gerezani. Michael Kamaliza na William Makori Chacha walihukumiwa kifungo cha miaka kumi kila mmoja.

Alfred Philip Milinga alifutiwa mashtaka yote, lakini hiyo ni baada ya kuwekwa kizuizini kwa miezi 16 chini ya Sheria ya Kizuizini wakati upelelezi wa kesi hiyo ulipokuwa unaendelea.

Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge kuiruhusu Serikali kuwakamata watu na kuwaweka kizuizini kama walidhaniwa kuhatarisha usalama wa taifa lakini ililalamikiwa na Jaji Mkuu wakati kesi hiyo ya uhaini ikiendelea.

Jaji Georges alilaumu kuwa sheria hiyo ilikuwa mbaya kwa sababu iliruhusu watu kushikiliwa kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani.

Kambona, ambaye alitajwa kuwa ni kiongozi wa uhaini huo, alihukumiwa bila yeye kuwapo mahakamani.

Hata hivyo, miaka saba baada ya hukumu ya kesi hiyo, Bibi Titi Mohamed aliachiwa huru kwa msamaha wa Rais Nyerere. Kitabu ‘Historical Dictionary of Women in Sub-Saharan Africa’ cha Kathleen E. Sheldon (uk. 155) kinasema Bibi Titi aliachiwa huru mwaka 1972.

Kitabu ‘Nyerere and Africa: End of an Era’ cha Godfrey Mwakikagile (uk. 373) kinasema walioachiwa pamoja na Bibi Titi mwaka 1972 ni pamoja na Eli Anangisye, ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu wa umoja wa vijana wa Tanu (Tanu Youth League) ambaye naye alikuwa amewekwa kizuizini akituhumiwa kuhusika na njama nyingine za kuipindua serikali ya Nyerere.

Mwaka 1977 alitoka gerezani mkoani Dodoma baada ya kudaiwa kuwa alimwandikia Rais barua ya kumwomba msamaha kwa yote aliyotenda.

Februari 5, 1978, Otini Kambona, ambaye ni ndugu yake Oscar Kambona na ambaye awali alikuwa Waziri wa Elimu na Habari, pamoja na Mattiya Kambona, waliachiwa huru kutoka gerezani pamoja na wengine 22 waliokuwa wametiwa kizuizini. Pia siku hiyo waliachiwa huru wafungwa wengine 7,000 kwa msamaha wa Rais.

Wote hawa waliachiwa huru katika maadhimisho ya kwanza ya kuzaliwa kwa CCM na miaka 11 ya Azimio la Arusha. Otini na Mattiya hawakufikishwa mahakamani na kwa sababu hiyo hawakuhukumiwa, bali walikuwa wamewekwa kizuizini ambako walikaa kwa miaka 10 tangu Desemba 1967 kwa sababu walikuwa wakimuunga mkono kaka yao, Oscar Kambona, na kwa kutumia gazeti alilomiliki la ‘Ulimwengu’ kuendesha propaganda za kisiasa.

Gazeti hilo lilikuwa likichapisha pia makala zilizoandikwa na Oscar Kambona akiwa uhamishoni Uingereza. Kambona mwenyewe hakuwahi kukamatwa, na wala hakukuwahi kufanyika jitihada zozote za kumrejesha nchini ili ashtakiwe pamoja na wale aliotuhumiwa kula nao njama.

Aliendelea kukaa nchini Uingereza hadi aliporejea nchini kwa hiari yake mwenyewe mwaka 1992 ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Itaendelea kesho...