Wahukumiwa kulipa fidia ya Sh40 milioni baada ya kukiri makosa

Tuesday October 8 2019

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wanne kulipa fidia ya Sh40 milioni baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya uhujumu uchumi.

Mbali na adhabu hiyo, washtakiwa hao walipewa adhabu ya kifungo cha nje kwa sharti na kutofanya kosa hilo tena na washirikiane na Serikali kutoa taarifa za watu wengine wanaojihusisha na makosa kama hayo.

Washtakiwa hao ni David Mudi, Mohamed Salum Mohamed, Mustapha Bakari, Salum Wakili na Shabani Haji wote wakazi wa Zanzibar.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Oktoba 8, 2019 na   Hakimu Mkazi,  Janet Mtega aliyebainisha kuwa washtakiwa hao  watalipa fidia hiyo  kwa utaratibu ulioonyeshwa katika hati ya makubaliano.

Washtakiwa hao ni miongoni mwa washtakiwa waliomwandikia barua kukiri na kuomba msamaha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa moja kwamba kati ya Novemba Mosi hadi 16,  2015 kati ya maeneo ya Zanzibar na Dar es Salaam walijihusisha na usafirishaji wa kobe 201 wenye thamani ya Sh30 milioni  bila kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.

Advertisement

 

Advertisement