Wakazi Dar watakiwa kujiandikisha daftari la wapigakura

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wananchi wa Mkoa huo kujiandikisha mapema katika daftari la kudumu la wapigakura si kusubiri hadi muda uishe na kuanza kulalamika.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wananchi wa Mkoa huo kujiandikisha mapema katika daftari la kudumu la wapigakura si kusubiri hadi muda uishe na kuanza kulalamika.

Akizungumza leo Jumatatu Februari 10, 2020 Makonda amesema shughuli ya uandikishaji katika Mkoa huo itaanza Februari 14 hadi 20, mwaka 2020 katika maeneo mbalimbali.

Amesema mbali na kujiandikisha wapo wanaotakiwa kuhuisha taarifa zao, wametakiwa kufika katika vituo vilivyoandaliwa na kwamba zaidi ya vituo 1600 vimeandaliwa kwa ajili hiyo.

“Hatutaki visingizio vya kuongezewa muda, fikeni mapema kwenye vituo vilivyo karibu huisheni taarifa zenu,  na kwa wale wanaoanza basi wajiandikishe ili mwisho wa siku wasikose haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wawatakao.”

“Uandikishaji huu unahusisha wale ambao wamefikisha miaka 18, lakini pia mtu labda ulihama mtaa au wilaya hakikisheni hampotezi haki yenu ya msingi,” amesema Makonda.

Pia, Mkaonda amesema Rais wa Tanzania, John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa wilaya mpya ya Kigamboni.

Kigamboni ni miongoni mwa wilaya mpya zilizoongezwa ikiwemo wilaya ya Ubungo na kufanya idadi ya wilaya katika jiji la Dar es Salaam kuwa tano.

Makonda amesema uzinduzi huo utafanyika katika jengo la ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo,  Sara Msafiri Februari 11, 2020.