KESI YA KINA KITILYA: Wakili ahoji waziri kutoshtakiwa kesi ya kina Kitilya

Dar es Salaam. Wakili wa utetezi katika kesi inayowakabili mkurugenzi wa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma), Harry Kitilya na wenzake amehoji sababu za aliyekuwa Waziri wa Fedha kutojumuishwa katika kesi hiyo na jibu la shahidi likawa “sijui”.

Majura Magafu anayemtetea Kitilya katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, aliibua hilo jana wakati akimhoji shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Grace Sheshui, ambaye ni kaimu mkurugenzi wa utawala na rasirimali watu wa Wizara ya Fedha Mipango kuhusu ushahidi wake.

Akijibu swali hilo na la ufafanuzi kutoka kwa wakili mwandamizi wa Serikali, Yemiko Mlekano, shahidi huyo Grace Sheshui alisema hajui ni kwanini waziri hajashtakiwa kwa kuwa hajui ni vigezo gani vilivyotumika kwa walioshtakiwa

Mbali na kamishna huyo mkuu wa zamani wa mamlaka ya mapato nchini (TRA), washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Immaculata Banzi, ni Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Shose ambaye amewahi kutwaa taji la Miss Tanzania mwaka 1996 na Solomoni walikuwa maofisa wa benki ya Stanbick. Shose alikuwa mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na uwekezaji, na Sioi alikuwa mwanasheria wa benki.

Shallanda na Misana walikuwa watumishi wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Shallanda akiwa kamishna wa sera na Misana akiwa kamishna msaidizi wa kitengo cha madeni cha idara.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58, baadhi yakiwa ni kuisababishia serikali hasara ya dola 6 milioni za Kimarekani, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo ya jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa dola 550 milioni kutoka benki ya Standard ya Uingereza.

Jana, Wakili Magafu alimuuliza maswali mbalimbali likiwemo chombo chenye mamlaka ya mwisho katika ukopaji serikalini, lakini shahidi huyo Grace Sheshui akajibu kuwa mwenye mamlaka ya mwisho ni Waziri wa Fedha na Mipango.

Kutokana na jibu hilo, Magafu alitaka kujua nani alikuwa Waziri wa Fedha mwaka 2012 na 2013 wakati wa mchakato wa mkopo huo.

Shahidi huyo alijibu kuwa wakati huo Waziri wa Fedha alikuwa Mustafa Mkulo na kwamba baadaye alifuatia Dk William Mgimwa (marehemu), na ndipo Magafu akahoji iwapo Mkulo ni miongoni mwa washtakiwa.

“Mkulo ni miongoni mwa washtakiwa? Unamuona hapa mahakamani miongoni mwa washtakiwa hao?” aliuliza Wakili Magafu na shahidi huyo akajibu kuwa hamuoni.

Pia akijibu maswali ya Magafu, shahidi huyo alisema anafahamu kuwa mbali na Waziri wa Fedha, kuna kamati mbili ndani ya wizara hiyo zinazoshughulika na masuala ya mikopo katika hatua za awali kabla ya mapendekezo kupelekwa kwa waziri ili kuidhinisha ukopaji.

Kamati hizo ni Kitaalamu ya Usimamizi wa Madeni (TDMC) ambayo mwenyekiti wake huwa ni kamishna wa sera na kwa wakati huo alikuwa mshtakiwa wa nne (Shallanda) huku katibu wake akiwa kamishna msaidizi wa madeni ambaye wakati huo alikuwa Misana (mshtakiwa wa tano).

Kamati nyingine ni Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa Madeni (NDMC) ambayo mwenyekiti wake huwa ni katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

TDMC hutoa ushauri wa kitaalamu kwa NDMC baada ya kupokea na kufanya uchambuzi wa kitaalamu wa mapendekezo ya mkopo kwa Serikali yanayowasilishwa na taasisi mbalimbali za kifedha.

NDMC ni kamati ambayo humshauri Waziri wa Fedha kuhusu mikopo ya ndani na nje.

Hata hivyo, alisema mapendekezo yaliyofanywa katika kikao cha 61 cha TDMC cha Septemba 18, 2012 kwenda NDMC, ambayo muhtasari wake umepokewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka na uliosainiwa na Misana hayakuwa mapendekezo yao washtakiwa hao pekee, bali yalikuwa ni ya kamati nzima.

Alipoulizwa na Wakili wa Serikali swali la ufafanuzi kuhusu swali la Wakili Magafu kuwa ni kwa nini watumishi hao wawili pekee ndio walioshtakiwa wakati waziri ambaye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho hajashtakiwa, alijibu kuwa hajui vigezo vilivyotumika kuwashataki hao wawili hao.