Wakulima watakiwa kutouza pamba chini ya Sh1,200

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wamewataka wakulima wa pamba kutokubali kuuza zao hicho chini ya bei elekezi ya Sh1,200.

 

Geita. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wamewataka wakulima wa pamba kutokubali kuuza zao hicho chini ya bei elekezi ya Sh1,200.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 21, 2019 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato  (CCU) pamoja na wananchi kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato kinachomilikiwa na CCU.

Amesema wakulima waendelee kuwa na subira kwa sababu wanunuzi hao wamepewa fedha za kutosha kununua pamba yote kwa bei hiyo, si vinginevyo.

“Hata mkiwa na shida msikubali kuuza pamba yenu chini ya Sh1,200 kwa kuwa haitachukua muda mrefu mtakuwa mmeshapata fedha zenu. Tuna taarifa kuwa kuna wanunuzi wamepata fedha na wanawatumia watu kwenda kuwalaghai wakulima kwa kutaka kununua kwa Sh800, msikubali na mkiwaona mtupe taarifa,” amesema Majaliwa.

Amesema viwanda vya nyuzi na nguo vikijengwa nchini kutakuwa na uhakika wa soko kwani hivi sasa Tanzania  haina viwanda vya kutosha vya nguo.

Amebainisha kuwa Serikali ipo tayari kuwaunga mkono Watanzania na mwekezaji  atakayekuwa tayari kuanzisha viwanda vya aina hiyo kwa sababu mahitaji ni makubwa.

Pia, amewaagiza viongozi wote wa vyama vya ushirika katika maeneo yanayolima pamba kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kuzalisha pamba safi ili walinde heshima ya pamba ya Tanzania ambayo duniani inasifika.

Awali, meneja wa CCU, Charles Nyasi alimueleza Majaliwa kuwa kampuni  ya METEL, KCCL na FRESHO zimejitokeza kununua pamba kupitia AMCOS na tayari kilo 9,611,860 zimenunuliwa  kati ya kilo 11, 140,529 zilizokusanywa.

Amesema kampuni ya FRESHO imenunua kilo 4, 869, 960; KCCL kilo 3, 025,051 na METEL kilo 1,716, 420.

Ameiomba Serikali  isaidie kuwalipia deni la Sh696 milioni ili kumaliza tatizo la madai ya watumishi na wadai wengine, “Pia Serikali isaidie kuilipia CCU deni la Sh102 milioni la ardhi waliyotumia kujengwa kiwanda chao.”

Akijibu maombi hayo, Majaliwa amesema Serikali haiwezi kulipa deni hilo hadi itakapopewa maelezo ya kina ni nani aliyelisababisha.