Walioambukizwa corona wafikia 20 Tanzania, wawili wapona

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema idadi ya watu waliopata maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania imefikia 20.
Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa leo Aprili Mosi imesema mtu mmoja raia wa Marekani amebainikiwa kuwa na virusi hivyo.
“Mgonjwa huyu ni raia wa Marekani mwenye miaka 42 ambaye amekuwa karibu na mtu aliyesafiri nje ya nchi na baadaye kuthibitika kuwa na maambukizi ya Covid 19 aliporejea nchini,” amesema Ummy.
Ummy amesema wagonjwa 17 wanaendelea na matibabu na hali zao ni nzuri na jana Machi 31 mgonjwa mmoja aliyekuwa katika kituo cha Temeke aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuthibitika kupona.
Hadi sasa Tanzania imekuwa na idadi ya watu wenye maambukizi ya virusi vya corona 20 huku wawili wakipona na mmoja kufariki dunia.
“Tunasisitiza wananchi kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalam wa afya katika kukabiliana na ugonjwa huo.”