Waliofariki dunia kwa corona Tanzania wafikia watatu

Muktasari:

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema watu wawili wamefariki dunia kwa ugonjwa wa corona na kufanya idadi ya waliokufa kwa ugonjwa huo nchini kufikia watatu.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema watu wawili wamefariki dunia kwa ugonjwa wa corona na kufanya idadi ya waliokufa kwa ugonjwa huo nchini kufikia watatu.

Amesema walioambukizwa  ugonjwa huo nchini sasa wamefikia 32 baada ya wagonjwa wengine saba  kuongezeka leo, wakiwemo wawili wa Zanzibar.

“Tunasikitika kutoa taarifa ya vifo viwili vilivyotokea leo miongoni mwa wagonjwa waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya corona nchini.”

“Waliofariki dunia ni mwanaume mwenye umri wa miaka 51  Mtanzania  mkazi wa Dar es Salaam tuliyemtolewa taarifa Aprili 8, 2020 na mwingine ni mwanaume mwenye umri wa miaka 57,” amesema Ummy.

Amesema wagonjwa hao watano, wanne ni wanaume wenye umri kati ya miaka 41 hadi 68 na mwanamke mmoja mwenye miaka 35.

“Leo Waziri wa Afya wa Zanzibar ametangaza uwepo wa wagonjwa wapya wawili waliothibitika kuwa na corona. Jumla ya waliothibitishwa kupata maambukizi ni 32. Kati ya hawa watano wamepona na wagonjwa wengine 24 wanaendelea vizuri na matibabu,” amesema Ummy.

Ameongeza, “vifo vimefikia vitatu tangu ugonjwa huu uliporipotiwa nchini. Kwa mara nyingine Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kama tunavyowapatia taarifa na elimu mara kwa mara kupitia njia mbalimbali.”

Mtu mmoja amefariki dunia tangu ugonjwa huo uliporipotiwa nchini.