Waliokamatwa kwa agizo la Makonda waachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Makandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Work wanaojenga barabara ya Banana –Kitunda na Chicco Engineering anayejenga daraja la Mto Ngo’mbe waliokamatwa jana Alhamisi Oktoba 24, 2019 kwa agizo la mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wameachia kwa dhamana.

Dar es Salaam. Makandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Work wanaojenga barabara ya Banana –Kitunda na Chicco Engineering anayejenga daraja la Mto Ngo’mbe waliokamatwa jana Alhamisi Oktoba 24, 2019 kwa agizo la mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wameachia kwa dhamana.

Wamepewa dhamana leo Ijumaa Oktoba 25, 2019 kutakiwa kwenda moja kwa moja katika maeneo ya kazi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katibu tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amesema licha kupewa fedha, wameshindwa kutekeleza kazi waliyopewa.

Jumanne Oktoba 22, 2019 Makonda alitangaza kuwapa siku tano makandarasi wanaosuasua kutekeleza miradi waliyopewa akitishia kuwakamata na kuwafukuza endapo hawatabadilika.

Leo Makonda amethibitisha makandarasi hao kuachiwa kwa dhamana akiwataka kwenda moja kwa moja kwenye maeneo yao ya kazi.

“Tumewapa dhamana ili wakafanye kazi. Tunataka kazi ifanyike, wenyewe wametuhakikishia kuwa wataongeza vifaa na ajira ili kazi ikamilike ndani ya miezi 10 badala ya 18 waliyopanga awali,” amesema  Makonda.