Waliokufa kwenye mafuriko Lindi wafikia 14

Muktasari:

Watu 10 wamekufa na wengine watano wa familia moja hawajulikani walipo baada ya mafuriko kuvikumba vijiji sita wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.

Kilwa. Watu 10 wamekufa na wengine watano wa familia moja hawajulikani walipo baada ya mafuriko kuvikumba vijiji sita wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.

Vifo hivyo vinafanya idadi ya waliokufa katika mafuriko wilayani humo kufikia 14, baada ya wengine wanne kuripotiwa kufariki jana.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 28, 2020 mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema hali si nzuri na uokoaji unaendelea katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko.

Mafuriko hayo yametokana na mvua iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo na kusababisha vijiji vya Kilanjelanje, Nanjilinji A, Ruatwe, Njinjo, Nakiu na Nanjilinji B kuzingirwa na maji.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema  hali sio mzuri  na shughuli ya uokoaji inaendelea katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko.

Amebainisha kuwa vikosi vya uokoaji vinaendelea na uokoaji,  hadi sasa watu1,531 wameokolewa kati ya wakazi 15,000 wa kijiji cha Njinjo kilichoathirika zaidi.

Akizungumzia mafuriko hayo kamishna wa operesheni na mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Liberatus Sabas amesema hali si shwari, unahitajika msaada kwa wananchi wa maeneo hayo.

“Ni kweli hali hapa sio mzuri juhudi  na nguvu kazi zinahitajika ili  kunusuru maisha ya wananchi,” amesema Sabas.