Wamiliki wa mabasi wamjia juu DC Sabaya kutoa tuhuma za jumla

Muktasari:

  • Taboa imemtaka mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kutotoa tuhuma za jumla kwa wamiliki wa mabasi kuwa wanahusika kuhujumu miundombinu ya Reli kati ya Moshi-Arusha, badala yake ashughulike na washukiwa kwa kufuata taratibu za kiuchunguzi.

Moshi. Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimemtaka mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya kutotoa tuhuma za jumla kwa wamiliki wa mabasi kuhujumu miundombinu ya reli.

Katibu mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema matamshi ya Sabaya katika vyombo vya habari yanawataja wamiliki wa mabasi kwa ujumla wao, badala yake ajikite na mshukiwa mwenyewe.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatatu Januari 20, 2020, Mrutu amedai matamshi ya Sabaya yanapeleka ujumbe mbaya kwa umma kwamba wamiliki wa mabasi wanapinga usafiri wa treni ya abiria.

“Treni ni ushindani wa kawaida kabisa ndiyo maana tunamtaka DC (mkuu wa wilaya) wa Hai asitaje wamiliki wa mabasi kwa ujumla wao. Kama kuna tuhuma basi tuviachie vyombo husika,” amedai.

Sabaya alipotafutwa na Mwananchi kwa simu yake ilikuwa haipatikani na hata ilipopatikana ilikuwa ikiita pasipo majibu na jitihada za kumtafuta azungumzie kauli hii zinaendelea.

Jana Jumapili Januari 19,2020 akikagua ukarabati wa njia ya reli ya Moshi-Arusha, Sabaya aliagiza kukamatwa kwa wamiliki wawili wa mabasi, akiwatuhumu kuunda genge la uhalifu kuhujumu miundombinu hiyo.

“Nimepata taarifa ambazo sihitaji kuzitilia mashaka kwa namna yoyote. Kwamba wakati nyinyi mnajenga reli hiii kutoka Moshi- Arusha kunao watu wameanza kuandaa magenge ya kihalifu,” amesema.

“Nimepata taarifa kuna watu wameanza kuja wanaanza kuchimba huku chini kutengeneza mashimo, kuweka mawe makubwa katikati ya reli lakini katika joint (kiunganishi) wameanza kulegeza nati.”

“Na wanaofanya kazi hiyo ni wamiliki na wafanyabiashara wa mabasi. Wanadhani kwa kufanya hivyo watawakatisha watu tamaa na biashara yao ya mabasi itaendelea kwa kasi zaidi,” alidai Sabaya.

Akiwa hapo kijiji cha Rundugai, Sabaya aliagiza mmiliki wa Machame Safari, Clemence Mbowe na mmiliki wa Lim Safari, Rodrick Uronu wawe wamejisalimisha polisi kufikia jana saa 12 jioni.

Wamiliki hao walipotafutwa na gazeti hili walikanusha vikali tuhuma hizo na kudai kushangazwa nazo wakisema haziwafananii, huku Mbowe akienda mbali zaidi na kudai ana wiki nzima yuko Dar es Salaam.