Wanajeshi 10 wa Tanzania wafariki kwenye mazoezi

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo

Muktasari:

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amesema sampuli za wanajeshi 10 waliokufa katika mazoezi ya kijeshi zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali  kwa ajili ya uchunguzi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amesema sampuli za wanajeshi 10 waliokufa katika mazoezi ya kijeshi zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali  kwa ajili ya uchunguzi.

Mabeyo ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 3, 2020  Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Januari 31, 2020.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli alitoa pole kutokana na vifo vya watu 20 katika kongamano wa Nabii na Mtume, Boniface Mwamposa vilivyotokea mjini Moshi, vifo vya watu 21 mkoani Lindi baada ya nyumba zao kusombwa na maji na vifo vya wanajeshi hao 10.

Mabeyo amesema wanajeshi hao walikuwa kwenye mazoezi ya kawaida ya kutembea.

Amesema baada ya saa mbili, hali zao zilianza kubadilika wakiwa eneo la Msata, walipelekwa hospitali ya Jeshi ya Lugalo.

Amesema baada ya kulazwa hospitalini hapo, baadhi yao walifariki na wengine hali zao ziliimarika. Amesema mpaka sasa kuna majeruhi watano.

"Tunahisi walikula chakula chenye sumu, labda wakati wanatembea walinunua vyakula barabarani vikawadhuru. Mazoezi yalikuwa ya kawaida tu.”

"Tumepeleka sampuli za waliofariki kwa Mkemia Mkuu ili kubaini chanzo hasa cha vifo," amesema Mabeyo akizungumzia vifo hivyo vilivyotokea Januari 30, 2020.