Wananchi wanaosotea vitambulisho vya Taifa wakata tamaa

Muktasari:

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi Januari 12,2020 laini zilizokuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole ni milioni 26 kati ya milioni 48. 

Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki siku tano kabla ya laini za simu ambazo zitakuwa hazijasaliwa kwa alama za vidole kuzimwa baadhi ya wananchi wamekata tamaa ya kufanikiwa kupata namba au vitambulisho vya Taifa ili wakamilishe usajili.

Hiyo ni kutokana na kile kilichobainishwa hata wakifanikiwa kukamilisha taratibu zote zinazohitajika watalazimika kusubiri kwa wiki tatu kabla ya kupata namba zao.

Hayo wameyasema leo Alhamisi Januari 16,2020 kwa nyakati tofauti katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi, Sharifu Mzurikwao ambaye ni mkazi wa Kisemvule amesema “hata nikihangaika kiasi gani sasa hivi siwezi kufanikiwa, nimeshajiandaa kisaikolojia kuwa lazima laini yangu itazimwa maana hakuna namna ninayoweza kufanya.”

Amesema leo ni siku ya tatu anarudi katika ofisi hizo kutokana na kila anapofika kuagizwa kuleta nyaraka zingine.

“Inataka moyo sana kwa kweli, unaweza kukata tamaa maana wakati mwingine unaombwa vitu ambavyo wewe mwenyewe hujui sehemu ya kuvipata ndiyo unaambiwa ukaape kwa mawakili,” amesema Mzurikwao

Roida Rekaby amesema wakati wakitangaza kusajili laini kwa alama za vidole alikuwa halipi uzito suala hilo lakini alijikuta akipata wasiwasi mara baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kutangaza kuongeza siku 20.

“Rais aliposajili ndiyo nikaona kumbe tutafungiwa kweli, nikaanza utaratibu wa kupata namba hizo lakini foleni ninayokutana nayo kila siku matumaini ya kufanikiwa kupata namba ndani ya muda yanafifia,” amesema

Desemba 27,2019 Rais Magufuli akiwa mapumziko nyumbani kwake, Chato mkoani Geita alitangaza kuongeza siku 20 zaidi kuanzia Januari1 hadi 20, 2020 baada ya hapo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) izime laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa.

Awali, TCRA ilitangaza mwisho wa matumizi ya laini zisizosajiliwa ingekuwa Desemba 31,2019.

Katika ofisi hizo za Nida Temeke, hofu hiyo haijaonekana tu kwa wale ambao hawajamaliza taratibu bali wengine wamekuwa wakifuatilia namba hizo kwa muda mrefu na hawajapata.

 

“Miezi miwili sasa tangu niandikishe nikija naambiwa namba bado haijatoka, sijui shida nini, inatukatisha tamaa maana kama namba imechukua muda huo kitambulisho si itakuwa miezi sita kabisa,” amesema Clementina Bujiko mkazi wa Mtoni Kijichi

Amesema licha ya kuambiwa namba itatoka baada ya wiki tatu imekuwa tofauti jambo ambalo limemfanya kila baada ya siku kadhaa kuacha shughuli zake kufuatilia namba hiyo.

“Ukija hapa siyo kwamba unaingia moja kwa moja kuulizia hapana usote kwenye foleni kama ni jua lako kama ni mvua yako ukifika kule unaambiwa bado,”

“Leo ndiyo ya mwisho nakuja kuulizia nikikosa basi nitatulia nyumbani hadi hizi vurugu ziishe ntakuja kwa muda wangu maana hata kwenye simu nimeuliza mara kadhaa sijaletewa,” amesema