Wanane hufa, 23 hujeruhiwa kila siku barabarani

Wednesday April 24 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Umewahi kupoteza hata dakika moja kufikiri namna unavyoweza kujilinda dhidi ya ajali za barabarani? Kama sivyo, tambua kila siku watu wanane hufariki dunia nchini kwa ajali hizo.

Kati yao, abiria wawili na waenda kwa miguu wawili hufariki dunia huku 15 wakiachwa na majeraha na baadhi kupoteza viungo.

Kwa miaka mitano mfululizo, takwimu hizo zinaonyesha abiria na waenda kwa miguu ni wanaathirika zaidi.Takribani abiria 964 walifariki dunia kutokana na ajali hizo huku zikiwaacha 4,238 wakijeruhiwa.

Mwaka 2018, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa takwimu zilizoonyesha kuwa watu takribani milioni 1.3 hufariki dunia kila mwaka huku kundi linaloathirika zaidi likiwa ni la abiria na waenda kwa miguu, hasa wa rika la miaka mitano hadi 29.

Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani (SACP), Fortunatus Muslimu amesema takwimu hizo ni za makundi ya watumiaji barabara kuanzia mwaka 2013 hadi 2018.

“Takwimu zinaonyesha kundi linaloathirika zaidi kutokana na ajali za barabarani ni abiria likifuatiwa na watembea kwa miguu na waendesha pikipiki,” alisema.

Advertisement

Kamanda Muslimu alisema watumiaji wa pikipiki wanachukua nafasi ya tatu kwa kuathirika kutokana na ajali za barabarani.

Kwa waenda kwa miguu, alisema vifo 854 na majeruhi 1,486 hutokea kila mwaka.

Makundi yaliyotajwa katika orodha hiyo ni pamoja na madereva, abiria, waendesha bodaboda, baiskeli, waenda kwa miguu na waendesha mikokoteni.

“Ndani ya kipindi cha miaka mitano ajali hizi zimesababisha vifo vya watu 14,853 kutoka katika makundi hayo, huku watu 42,106 wakiachwa na majeraha mwilini,” alisema Muslimu.

Mabadiliko ya Sheria

Kamanda Muslimu alisema bado kuna mkanganyiko mkubwa katika sheria ili kuweza kupunguza ajali hizo za barabarani.

“Sheria inaeleza watoto chini ya miaka 12 wakiwa wawili kwenye gari wanajumuishwa kuwa ni abiria mmoja, hii inaleta mkanganyiko kwenye usimamizi. Unaweza kuona gari ya shule imejaa na imezidi kupita kiasi lakini kutokana na sheria, ndani kuna watoto 80 lakini inahesabika 40, hiyo inatufanya tushindwe kuzichukulia hatua gari zinazoweka watoto zaidi ya wawili kwenye siti mbili,” alisema.

Akieleza mchakato wa sheria, Muslimu alisema mapendekezo yatapelekwa Baraza la Mawaziri na utaandikwa muswada kwa ajili ya kupelekwa bungeni, “niseme tu tumeyapitia kwa kushirikiana na wadau wamebaini ombwe lililopo katika kuhakikisha kwamba sheria yetu inaboreshwa zaidi.”

Mwenyekiti wa mtandao wa wabunge wa masuala ya usalama barabarani Tanzania, Adadi Rajabu alisema bado kuna haja ya kuwa na sheria mpya kwa kuwa upande wa elimu, sheria na adhabu umeelezwa kuwa na upungufu mkubwa katika sheria ya sasa.

“Sheria ile ina mapungufu lakini huwezi kufanya chochote mpaka iletwe bungeni. Je, Serikali inayaona yale mapungufu, marekebisho haya yamewahi kuzungumziwa muda mrefu na hili limekuwa likisubiriwa kuona tutarekebisha kwa namna gani,” alisema Adadi.

Alisema sheria kali zinatakiwa zitengenezwe ili kuhakikisha ajali zinapungua kwa kiasi kikubwa, kwani tatizo si tu kumuadhibu mhusika, bali kuhakikisha anakuwa na uelewa.

Alisema adhabu zikiwekwa kali kwa mujibu wa sheria kila dereva atakuwa makini barabarani kwani atakuwa anajua wazi akifanya kosa atakumbana na adhabu kali.

“Atajua, kwa mfano akisababisha ajali na ikasababisha kifo, akiendesha gari huku amelewa, hajafunga mkanda, basi adhabu ni jela moja kwa moja.

“Niliwahi kwenda nchini Japan, kule wana adhabu kali tena ukienda mtu mgeni wanakuambia wazi kwamba kuna mambo mawili, huruhusiwi kuendesha gari kama huna kibali maalum na ikiwa utapata ajali unaishia kwenda jela maisha.

“Kwa hiyo kila nchi ina sheria zake, hivyo nasi lazima tuangalie sheria zetu je! zipo sawa sawa na zinamfanya mtu akishika gari kujua kwamba ameshikilia uhai wa watu?” alihoji.

Advertisement