Wanaodahili wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya Tanzania wapewa miezi mitatu

Muktasari:

Tume ya Vyuo Vikuu nchini Tanzania (TCU) imetoa miezi mitatu kwa mawakala wanaodahili wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya nchi kujisajili waweze kutambulika.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu nchini Tanzania (TCU) imetoa miezi mitatu kwa mawakala wanaodahili wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya nchi kujisajili waweze kutambulika.

Tume hiyo imeandaa miongozo ya uanzishwaji na uendeshaji wa mawakala hao kwa ajili ya  kudahili wanafunzi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Januari 28, 2019 Katibu mtendaji TCU,  Profesa Charles Kihampa amesema mawakala watatu kati ya sita ndio wamejisajili.

“Wakala ambao wamesajili ni Global Education Link, Darwin Education Agency LTD na Yuhoma Education LTD, wanatakiwa kuhuisha usajili wao kila baada ya miaka mitatu,” amesema.

Amesema Januari 2020 tume hiyo imepokea maombi ya mawakala wengine saba, taratibu za usajili zinaendelea.

Amesema kwa takribani  miaka 12 kumekuwa na mawakala wanaodahili wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya Tanzania, kwamba jukumu la TCU ni kuwasajili.

“Utekelezaji wake haukuwahi kufanyika kwa sababu ya kukosekana kwa miongozo ya namna bora ya kuzitambua na taratibu za uendeshaji.”

“Wakala wote ambao hawajasajili wanahimizwa kutuma maombi yao TCU na kukamilisha taratibu za usajili kwa wakati, ifahamike kuwa kuendesha wakala wa kudahili wanafunzi bila usajili ni kinyume cha kanuni ya 47 (1) (d) na (f) ya kanuni za vyuo vikuu za mwaka 2013,” amesema.

Ameeleza hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji na majukumu ya tume hiyo katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2015.