Wanaodaiwa kuwateka NCCR mbaroni

Muktasari:

Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama alikiri kuwapo kwa tukio hilo ingawa bado hajapata ukweli kamili wa tukio hilo.

Moshi. Watu watatu wanaoshukiwa kuwateka na kuwatesa makada wawili wa chama cha NCCR-Mageuzi katika Jimbo la Vunjo wametiwa mbaroni katika ukamataji ulioonekana kama sinema.

Mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia NCCR-Mageuzi, James Mbatia alilazimika kufukuzana na gari lao aina ya Toyota Prado kwa saa kadhaa kabla ya kupata msaada wa polisi waliofunga barabara.

Wakati hayo yakiibuka Moshi, kamanda wa polisi mkoani Geita, jana aliliambia Mwananchi wanaendelea kuwasaka wanaotuhumiwa kuvamia nyumbani kwa mgombea ubunge wa Chato kupitia Chadema, Michael Masai na kufanya uharibifu

Kwa mujibu wa mashuhuda, gari hilo lililosajiliwa kwa namba za mashirika (DFP), lilisimamishwa na polisi maeneo matatu tofauti lakini halikusimama.

Hata hivyo, polisi ambao walikuwa wakiwasiliana, waliamua kufunga barabara ya Moshi-Himo katika eneo la KDC na kuwatia mbaroni watu watatu huku wa nne akitoroka.

Baada ya kukamatwa, walijitambulisha kwa polisi kuwa wao ni maofisa usalama wa Taifa na wakawa hawataki kwenda polisi hadi ofisa usalama wa Taifa mmoja anayetambulika alipowathibitishia polisi kuwa watu hao si maofisa usalama wenzake.

Baada ya gari hilo kufikishwa polisi saa 11 jioni na kupekuliwa, lilikutwa na mikasi, bisibisi, marungu, jambia, kinyago (face mask), mitalimbo na vibao vinne tofauti vya namba za usajili wa magari.

Septemba 17, saa 1 usiku, watu waliojitambulisha ni polisi wakiwa na gari aina ya Toyota Prado waliwateka makada wawili wa NCCR-Mageuzi katika Kijiji cha Mkyashi huko Kilema.

Makada hao, Yolanda Lyimo anayegombea udiwani wa viti maalum na Deogratius Mosha ambaye ni meneja kampeni wa chama cha NCCR-Mageuzi, wanadaiwa kuteswa na Deogratius kukatwa sikio kabla ya kutupwa msituni.

Taarifa zinasema Jumapili ya Septemba 27, gari hilo linadaiwa kwenda Marangu na watu waliokuwamo ndani walishuka na kujitambulisha kuwa ni polisi wakitaka kuwakamata vijana wa NCCR-Mageuzi.

Hata hivyo, makada hao waliwatilia mashaka ikizingatiwa kuna taarifa za kutekwa kwa wenzao na watu waliokuwa kwenye Toyota Prado hivyo kusababisha kutokea kwa purukushani zilizosababisha watu hao kukimbia.

Kamanda wa polisi Mkoa Kilimanjaro, Emanuel Lukula alipofuatwa na mwandishi wetu ofisini kwake, hakuwa tayari kuongea naye hata pale mwandishi alipomsihi afanye hivyo kupitia kwa Afisa Mawasiliano wake.

Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama alikiri kuwapo kwa tukio hilo ingawa bado hajapata ukweli kamili wa tukio hilo.

“Tukio nalijua ila linafanyiwa uchunguzi, taarifa hazijakaa sawa. Bado sijapata ukweli wote, kuna mkanganyiko wa mambo na sitaki kuliongelea kwa sasa nasubiri taarifa sahihi kutoka kwa mtu niliyemwagiza alichunguze,” alisema.

Mbatia aeleza mwanzo mwisho

Mbatia alisema saa nane mchana juzi kulikuwa na gari aina ya Toyota Prado lililokuwa linawafuatilia akiwa Moshi mjini hivyo wakaamua kubadilisha njia na kuliacha liwatangulie nao wakilifuata kwa nyuma.

“Tulilihisi gari hilo ndilo linafanya matukio ya kihalifu. Tarehe 27. 09. 2020 gari hilo lilikwenda Marangu, wakajitambulisha ni polisi na wakatoa vitambulisho wakataka kuwakamata vijana wetu,” alidai Mbatia.

Alisema baadaye gari hilo lilienda mji mdogo wa Himo ambako lilibadili uelekeo na kurudi Moshi na wao wakalifuatilia wakati huku Mbatia akiwasiliana na polisi wa Kilimanjaro na makao makuu.

“Tulipofika Sango (Moshi) walisimamishwa na trafiki wakakataa kusimama na kutaka kuwagonga ikabidi askari waruke pembeni kuokoa maisha yao. Tuliendelea kulifukuza pamoja na polisi,” alidai.

“Tulipofika KDC gari la polisi aina ya Hyundai likasaidia kulisimamisha lile gari lakini wakapita pembeni. Baadaye yalikuja magari mengine ya polisi aina ya Toyota Landcruiser yakiwasha vimulimuli ndiyo yalifanikiwa kuwadhibiti.”

“Nalishukuru Jeshi la Polisi wamefanya kazi nzuri sana ya kupigiwa mfano maana wale jamaa walikuwa wanawatishia polisi kuwa wao ni maofisa usalama wa Taifa lakini polisi walikomaa nao,” alisema mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi Taifa.

Mbatia alisema aliwasiliana na uongozi wa usalama mkoani Kilimanjaro ambao walimtuma ofisa usalama wilaya (DSO) ambaye aliwathibitishia polisi kuwa watu hao hawakuwa maofisa wa taasisi hiyo nyeti ya umma.

Tukio la kukamatwa kwa washukiwa hao limekuja siku chache baada ya makada wawili wa Chadema Jimbo la Hai nao kudaiwa kutekwa kisha kuteswa na baadaye kutupwa mkoani Arusha.

Miongoni mwa mateso waliyofanyiwa ni kuminywa korodani kwa koleo, kung’olewa meno kwa koleo, kukatwa sikio na kupigwa shoti ya umeme.

Makada hao walitekwa juzi wakiwa Kata ya Narumu na watu waliokuwa na magari matatu ya kiraia wakidaiwa kuwa na bunduki mbili na bastola moja.

Baada ya kuwatesa wmateka wao, waliwatupa maeneo tofauti wilayani Arumeru kishakutokomea kusikojulikana hivyo kuliongezea jukumu Jeshi la Polisi ya kuwasaka popote walipo.