Wanaotaka fedha kutoa vyeti vya kuzaliwa waonywa

Muktasari:

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga amewaonya watendaji wanaowatoza wazazi  fedha ili kuwasajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Morogoro. Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga amewaonya watendaji wanaowatoza wazazi  fedha ili kuwasajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Zaidi ya watoto milioni 3.7 katika mikoa 15 nchini wameandikishwa na kupatiwa vyeti hivyo kupitia mpango  unaolenga kuwafikia watoto wote walio chini ya umri huo.

Usajili huo unafanywa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Watoto Duniani (Unicef) na kampuni ya mawasiliano ya Tigo.

Mahiga ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 11, 2019 wakati akizungumza  kwenye uzinduzi wa mpango wa usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano mkoani  Morogoro na Pwani.

Mahiga amesema amepata taarifa kuwepo kwa baadhi ya wasajili walioanza kujinufaisha na mpango huo kwa kuwatoza   fedha wazazi wenye watoto wanaotaka kuwasajili.

“Usajili ni bure kabisa na wasajili wasitumie fursa hii kupata kipato, vyomvo vya ulinzi na usalama viwakamate watakao potosha dhamira hii ya Serikali,” amesema Mahiga.

Awali ofisa wa kitendo cha ulinzi wa mtoto cha Unicef, Maud Fortuyn amesema kusajili watoto baada ya kuzaliwa ni haki yao ya msingi inayosaidia watambuliwe jina, wazazi na mahali wanapoishi.

Kaimu mtendaji mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita),  Emmy Edson amesema katika mikoa ya Pwani na Morogoro kampeni ya usajili huo itafanyika kwa siku 12 kwenye  ofisi za kata na vituo vya afya.