Wanasiasa Tanzania wanavyozungumzia miaka miwili ya Tundu Lissu kushambuliwa

Muktasari:

  • Leo Jumamosi aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametimiza miaka miwili tangu aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa demokrasia wametoa salamu za pole na hongera kwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu wakikumbuka miaka miwili tangu aliposhambuliwa na risasi na watu wasiojulikana.

Lissu tangu aliposhambuliwa zaidi ya 30 Septemba 7, 2019 nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma ambaye ametumia muda wote huo akipata matibabu nje ya nchi ya Tanzania.

Baada ya shambulizi hilo, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyo hiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipotibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambako yuko huko hadi leo.

Ikiwa pamoja na Kenya na baadaye nchini Ubeligiji kwa sasa amefungua kesi Mahakama Kuu kupinga kuvuliwa ubunge Juni 28, 2019 na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Akitangaza uamuzi huo wakati wa kuahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitaja mambo mawili yaliyomponza Mnadhimu Mkuu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa ni kutojaza taarifa za mali na madeni na sababu ya pili kutotoa taarifa kwa Spika mahali alipo.

Baadhi ya wanasiasa wametuma ujumbe kwenye mitandao ya jamii kuzungumzia tukio hilo na miongoni ni Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na mwanachama wa chama hicho, Ismail Jussa.

Katika ujumbe wa Zitto unaozungumzia tukio hilo anasema mapito aliyopita Lissu siku hiyo hakuna mtu anatamani kupita.

“Nchi nzima ilitaharuki. Macho na masikio yakawa General Hospital Dodoma na baadaye Nairobi kisha Leuven, Belgium. Mbunge kushambuliwa na risasi saa saba mchana akiingia nyumbani haijapata kutokea Tanzania," amesema. 

Amehoji sababu za kutokamatwa kwa watu waliomshambulia Lissu baada ya miaka miwili huku Lissu mwenyewe akinyimwa matibabu: “Kazushiwa kila aina ya propaganda na sasa kavuliwa ubunge. Ukatili ambao haumithiliki.

“Wenzangu waliniuliza mbona umekuwa mkali sana post Septemba 7, 2017? Nikawaambia kuwa lengo la waliomshambulia Lissu ni kutunyamazisha. Tukinyamaza watakuwa wameshinda. Sasa sote twapaswa kuwa Tundu Lissu ili kutowapa ushindi watu katili na dhalimu. Mwenendo wa siasa ulibadilika.”

Mbali na Zitto, mwanahabari Maria Sarungi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa tukio la kupigwa risasi Tundu Lissu ni tukio la kihistoria.

“Pia, ni tukio lililoweka alama katika saikolojia ya Taifa. Ilikuwa kitendo cha kikatili na kuweka bayana uovu ambao hatujawahi kufikiri unawezekana ndani ya nchi yetu,” amesema Sarungi.

Kada wa chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa pia ameandika katika Twitter akisema: “Ni miaka miwili. walikusudia wakuue, Mwenyezi Mungu akakataa. Wengi tunaamini Mungu amekunusuru na amekubakisha hai kwa sababu kuna kazi unapaswa kuifanya. Tunaamini wewe utakuwa sababu ya kuifikia Tanzania yenye haki na yenye neema kwa watu wake wote.”

Mbunge wa viti maalumu wa Chadema, Catherine Ruge pia ameandika katika Twitter akisema: “Siku hiyo giza lilitanda nchi nzima kwani tukio kama hili halijawahi kutokea nchini kwetu. Waliotaka kumuua wameshindwa, leo hii Lissu is still standing still. Glory to God (utukufu kwa Mungu).”