Wapongeza mchango wa Serikali kuinua Sekta Binafsi

Muktasari:

Wafanyabiashara wa sekta binafsi wamekutana kumpongeza Rais John Magufuli kwa mafanikio ndani ya uongozi wake wa miaka mitano

Dar es Salaam. Wakati miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano ikielekea ukingoni wafanyabiashara wa Sekta Binafsi wamempongeza Rais John Magufuli kwa namna alivyoiinua sekta hiyo katika nyanja mbalimbali.

Wakizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) leo Oktoba 18, wafanyabiashara hao wameeleza kuwa Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kuiinua sekta hiyo.

 

Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabishara wadogowadogo (Vibindo Society), Gaston Kikui amesema miaka mitano iliyopita imekuwa ya heri kwa upande wao.

“Tunampongeza Rais kwa kazi nzuri hasa ya kuwajali wafanyabiashara wadogowadogo. Tulimshauri kuhusu vitambulisho vya wamachinga ambavyo vimekuwa msaada mkubwa.

Ameweza kuwasaidia wavuvi wa feri kujenga ofisi na mama lishe kutengenezewa eneo zuri kwa ajili ya biashara yao. Tunachotaka sasa   soko la mabibo tupewe wafanyabiashara tuliendeshe wenyewe,” amesema.

 

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waendesha bodaboda Tanzania, Michael Haule alishukuru kwa kupata bima ya afya ya gharama nafuu kwa waendesha bodaboda.

“Inafahamika kuwa waendesha bodaboda ajali ni sehemu ya kazi yetu, hivyo kutupa bima ya bei nafuu ni kuturahisishia maisha na kutuweka salama wakati wote.

Kwenye sekta ya afya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha watoa huduma za afya Tanzania (Aphta), Dk Samwel Ogilo amesema changamoto nyingi zilizokuwa zinawasumbua zimepatiwa ufumbuzi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano sekta ya afya imekuwa na uwekezaji mkubwa na ongezeko la vituo vipya vya afya.