Washtakiwa kesi ya bomba la mafuta waendelea kusota rumande

Muktasari:

  • Jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia (Tazama), Samwel Nyakirang'ani (63) na wenzake 11, lipo katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kuchambuliwa

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia (Tazama), Samwel Nyakirang'ani (63) na wenzake 11, lipo katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP) kwa ajili ya kuchambuliwa.

Washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kwa muda wa miezi 11 na siku 18 sasa, kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 16, 2018 kujibu mashtaka matatu likiwemo la kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA),  lakini hadi sasa upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita amedai leo  Januari 4, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega, kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa.

Mwita ameeleza kuwa jalada la shauri hilo lipo ofisi ya DPP kwa ajili ya kuchambuliwa na kulitolea maamuzi  hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha  kesi hiyo hadi Januari 16, 2019 itakapotajwa.

Washtakiwa wote wapo rumande kutokana DPP kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana.

Mbali na Samweli, washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 1/2018 ni Nyangi Mataro (54) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Ufukoni.

Wengine ni mfanyabiashara, Farijia Ahmed (39), Malaki Mathias (39), Kristomsi Angelus (25), Pamfili Nkoronko (40) na Henry Fredrick (38), Audai Ismail (43), Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Kwa pamoja wanadaiwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilayani Kigamboni, washtakiwa wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali.

Katika shtaka la pili ambalo ni kuharibu miundo mbinu, inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walitoboa bomba la hilo ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta mali ya TPA.

Pia wanadaiwa kuharibu bomba la mafuta mazito lenye upana wa inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali ya TPA.