Watu 10 wafa maji wilayani Sengerema

Muktasari:

Watu 10 wamekufa maji baada ya nyumba walizokuwa wakiishi  kusombwa na maji katika kata ya Nyatukala wilayani Sengerema.


Sengerema. Watu 10 wamekufa maji baada ya nyumba walizokuwa wakiishi  kusombwa na maji katika kata ya Nyatukala wilayani Sengerema.

Nyumba hizo zilikuwa jirani na mto uliojaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 23, 2019 mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amesema, “watoto wa kiume watano na wanawake watano miili yao ndio imepatikana na imehifadhiwa hospitali ya Wilaya ya Sengerema.”

Amesema matukio ya aina hiyo hutokea mara kwa mara wilayani huyo, akibainisha kuwa wanatumia kamba na nyavu kutafuta miili mingine.

“Watu wanapaswa kujihadhari kujenga karibu na mto kwa kuwa ukijaa maji husomba nyumba,” amesisitiza Kipole.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa waokoaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu,  Revocatus Kayanga amesema wanaendelea na uokoaji kwa maelezo kuwa huenda kukawa na miili zaidi.