Watu wasiojulikana waiba vifaa vya Nida, DC Muro atoa maagizo

Muktasari:

 Watu wasiojulikana wameiba vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) huku mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro akitoa angalizo kwa wananchi  kutokununua vifaa hivyo kwani wakikamatwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Arusha. Watu wasiojulikana wameiba vifaa vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha nchini Tanzania.

Mkuu wa wilaya Arumeru, Jerry Muro amesema wizi huo umetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 6, 2020 katika ofisi za Nida zilizopo jengo la halmashauri ya Wilaya ya Arusha (DC).

Muro amesema vifaa vilivyoibwa ni kamera mbili, stendi mbili, kompyuta mpakato mbili, kompyuta moja (Desk top), stendi mbili, Extation mbili, keyboad moja na Damalog moja.

"Kutokana na wizi hii, jeshi la polisi linawashikilia watu wawili  ambao ni mlinzi Asheri Lorubani na muhudumu wa ofisi, Wilson Laizer," amesema

Muro amesema ameagiza vyombo vya usalama kuchunguza tukio hilo ili wote waliohusika wachukuliwe hatua.

"Tunaomba wananchi watupe taarifa nawaomba wasinunue kamera mtaani, kompyuta ama vitu vilivyoibwa kwani ukikamatwa ni sawa na kununua nyara za Serikali," amesema

Amesema hii si mara ya kwanza wizi kutokea katika ofisi za Nida Arumeru ulitokea mara ya kwanza bado upelelezi unaendelea kwani hii ni hujuma dhidi ya wilaya.

Akizungumzia na Mwananchi, Mkuu wa Nida wilaya ya Arumeru, Neema Nkya amesema leo asubuhi wamefika ofisini na kukuta vifaa hivyo vimeibwa.

Nkya amesema hata hivyo wezi hawajavunja ofisi na wameshangazwa na wizi huo kwani umeathiri shughuli ya utoaji vitambulisho katika wilaya hiyo.

Kamanda wa polisi  mkoa Arusha Jonathan Shana amethibitisha kuripotiwa tukio hilo na kueleza upelelezi umeanza na itatolewa taarifa rasmi ya polisi