Wauza vinyago walalama biashara yao kudoda, wataja sababu

Sunday December 8 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imewatoa wasiwasi wafanyabiashara wa vinyago kuhusu taratibu za usafirishaji wa bidhaa kwa wageni wanapoondoka nchini.

Kwa muda mrefu wafanyabiashara hao wamekuwa na malalamiko kuwa wakala hao wamekuwa kikwazo cha wao kuuza vinyago kutokana na usumbufu wanaokutana nao wageni wanapopita na vinyago katika uwanja wa ndege.

Akizungumza wakati wa mkutano kati ya wafanyabiashara wa vinyago wa Mwenge na maofisa wa wakala hao, Meneja wa TFS wilaya ya Kinondoni Dotto Ndumbikwa amesema kinachofanyika ni kuhakikisha rasilimali za misitu zinasimamiwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Amesema si lengo la TFS kuwakwamisha bali wanataka biashara hiyo ifanyike kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuhusisha vibali kwa vinyago vinavyozidi kilogramu 10 vinaposafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Tumekuja kuzungumza nao na kuwapa ufafanuzi waelewe kwamba pale uwanja wa ndege kinyago chochote ambacho kitakuwa chini ya kilo 10, hakitatakiwa kukatiwa kibali ila kiasi hicho kimezidi utaratibu uliopo ni lazima kiwe na kibali,”

Kurahisisha hilo tumefungua ofisi hapa Mwenge ili vibali na nyaraka zingine ziweze kupatikana hapa na kumuondolea usumbufu mgeni anapofika uwanja wa ndege na kukutana na maelekezo yanaweza kumsababishia kuacha vinyago alivyobeba,”

Advertisement

Amesema, “Endapo mgeni aliyenunua kinyago na kupata vibali kutoka katika ofisi yetu ya Mwenge hakuna ofisa wa TFS anaweza kumsumbua labda vishoka wanaofanya hivyo kwa maslahi yao binafsi.”

Mwenyekiti wa wachonga vinyago wa Makonde Crafters Hamis Mhando alisema wamekuwa wakipoteza wateja wa vinyago kutokana na wageni kushindwa kuhimili usumbufu wanaokutana nao uwanja wa ndege wakitakiwa kutozwa.

“Sasa hivi hatuna biashara wageni wameambizana wakija Tanzania hawanunui vinyago kutona na usumbufu wanaopata kutoka kwa watu wa maliasili pale Airport. Imekuwa changamoto kubwa kwetu tunatengeneza vinyago na kukaa navyo tunaomba serikali iliangalie suala hili,” amesema Mhando.

Advertisement