VIDEO: Wazazi walivyohama kijiji kumtafutia shule mtoto wao mwenye ulemavu

Baadhi ya watoto wenye ulemavu wamekuwa wakipitia changamoto nyingi zikiwemo kufichwa ndani ya nyumba, kunyimwa haki ya kupata elimu na kuchangamana na wenzao. Kibaya zaidi haya yanafanywa na wazazi au walezi wao.

Hata hivyo, kwa wazazi wa Pili Mandai (10) hili wamelishalitoa katika fikra zao. Kwa aina ya ulemavu wake na ugumu wa maisha walionao wazazi, Pili angekuwa mtu wa kufichwa ndani, lakini leo yupo masomoni akisoma katika Shule ya Msingi Lukolongo iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Si tu Pili yuko masomoni kwa sasa, lakini wazazi wake walilazimika kuhama makazi kutoka Kijiji cha Namawala kilichopo Wilaya ya Ifakara na kwenda Kijiji cha Mngeta kilichopo Kilombero ili tu kusaka kijiji ambacho kina shule yenye watoto wenye mahitaji maalumu

Akizungumza katika hafla ndogo ya kukabidhiwa baiskeli kwa Pili, baba mzazi wa Pili, Ayubu Mandai anasema walilazimika kufanya hivyo ili mtoto wao aweze kusoma katika shule yenye miundombinu rafiki.

Simulizi ya Pili

Mandai anasema kuwa baada ya Pili kuzaliwa wakiwa wanaishi Namawala walimpokea kwa shingo upande, lakini hawakuwa na namna zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na ilipofika umri wa kuanza shule ya awali walianza kumpeleka shule.

“Tulikuwa tukipangiana zamu, mke wangu yeye alikuwa akimwandaa asubuhi na mimi nilikuwa na kazi ya kumpeleka shuleni asubuhi na saa tano namfuata kwa kumbeba katika baiskeli ya magurudumu mawili,’’ anasema.

Alipofika darasa la kwanza mwaka jana walipata taarifa ya kuwapo kwa shule ya msingi yenye kitengo cha watoto wenye ulemavu iliyopo Mngeta, hivyo wakashauriana na mke wake na kufikia uamuzi wa kuhama ili wapate urahisi wa kumsaidia mtoto wao.

“Tunachoweza kushukuru baada ya kuhamia Mngeta ni kuunganishwa na wasamaria wema ambao wamemsaidia Pili baiskeli ya magurudumu matatu ambayo itamsaidia kwenda shule mwenyewe na sisi wazazi wake kupata nafasi ya kufanya shughuli za maendeleo kwa uhuru tofauti na hapo awali ambapo muda mwingi tulilazimika kumwangalia yeye,’’ anaeleza.

Mama wa Pili, Dalini Chobo anasema mwanawe ameshamueleza kuwa ana ndoto ya kuja kuwa mwalimu katika maisha yake.

“Pili ana shauku ya kuwa mwalimu baada ya kumaliza masomo yake na kuwafundisha wenzake. Hiyo ndio ndoto yake amekuwa akinieleza,” anasema.

Anasema amekuwa akichelewa kufanya kazi nyingine kwa ajili ya uangalizi wa mtoto huyo hasa asubuhi ili aende shule na imefikia hatua ya kupokezana majukumu yeye na mume wake.

“Maisha kule Namawala hayakuwa mazuri kwetu kutokana na kutegemea kipato kutoka kwenye kilimo, lakini kilimo chenyewe huwezi kulima kwa asilimia 100. Hapa Mngeta tutajikita zaidi kwenye kilimo,’’ anasema.

Anachokisema Pili

Pili anataka kuwa mwalimu wa shule ya msingi ili apate nafasi ya kuwafundisha wanafunzi wa madarasa ya awali (Chekechea) na darasa la kwanza.

Anasema anayatamani madarasa hayo kwa sababu amegundua kuwa kundi kubwa la wanafunzi wanaingia darasa la kwanza hadi la pili wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Na yeye anataka kuwa sehemu ya kutatua changamoto hiyo.

“Navutiwa na kazi ya kufundisha watoto wa shule za chekechea na darasa la kwanza kwani nataka wajue kusoma na kuandika katika madarasa hayo ili wakifika madarasa ya mbele wasiwe na shida katika kusoma vitabu, kuandika na kuhesabu,” anasema Pili.

Anasema anapitia changamoto nyingi za kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine na amekuwa akitamani kucheza kama wanavyocheza wenzake, lakini baada ya kupata baiskeli ya magurudumu matatu atakuwa na fursa kumuwezesha kutembea akitumia chombo hicho.

“Nimekuwa nikipata maumivu katika magoti hasa ninapotoka sehemu moja kwenda nyingine, kwani mimi natembea kutumia magoti. Nikitembea sehemu ya ardhi ngumu imekuwa ikiniumiza hata wakati wa kwenda chooni pia,’’ anaeleza Pili aliyekabidhiwa baiskeli hiyo na wasamari wema wakiongozwa na mwandishi wa makala haya.

Anasema kuwa choo anachotumia ni choo kinachotumiwa na wanafunzi wengi, hivyo kumekuwa na hali ya uchafu jambo ambalo si rafiki kwake kutokana na mazingira anayoishi.

“Ili kufikia malengo ya kuwa mwalimu nahitaji kupambana zaidi darasani ili niweze kusoma kwa bidii, lakini naona kama naweza kukwama kwa kukosa vifaa vya shule kama madaftari, vitabu, sare za shule na viatu kutokana na hali ya mazingira ya wazazi wangu sio nzuri sana,’’ anasema.

Mwalimu mkuu azungumza

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Lukolongo, Chomela Mondo anasema shule hiyo ina wanafunzi wenye ulemavu 38 wakiwa na ulemavu wa uoni hafifu, uziwi, mtindio wa akili na ulemavu wa viungo.

Mondo anasema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika shule hiyo ni kuwa na mwalimu mmoja pekee mwenye mafunzo maalumu ya wanafunzi wenye ulemavu