Waziri Biteko abaini kiwanda bubu uchenjua madini, atoa maagizo kwa polisi

Muktasari:

  • Waziri wa Madini nchini Tanzania, Doto Biteko amebaini uwapo wa kiwanda bubu cha uchenjuaji wa madeni mkoani Shinyanga na kuagiza polisi mkoani humo kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.

Kahama. Waziri wa Madini nchini Tanzania, Doto Biteko amewaagiza polisi mkoani Shinyanga kumkamata na kumhoji ofisa mtendaji wa kijiji cha Bunango kata ya Bugalama Halmashauri ya Msalala, Kanjanja Kanjanja baada kuhusishwa kushirikiana na watoroshaji wa madini ya dhahabu kwa kufungua kiwanda bubu cha uchenjua wa madini.

Pia, amewaagiza kukamatwa kwa mmiliki wa nyumba ambayo imefungwa kiwanda hicho pamoja na wamiliki wa kiwanda hicho ili waweza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa makosa ya utoroshaji wa madini kwa kufungua kiwanda bubu.

Biteko alitoa maagizo hayo jana Jumatano Januari 1, 2020 wakati wa ziara ya kushtukiza katika moja ya nyumba iliyopo katika kijiji cha Bunango kata ya Bugalama na kubaini kuwapo kwa kiwanda bubu cha uchenjuaji wa madini ambacho kilianza uzalishaji tangu Julai mwaka 2019.

Alisema ofisa mtendaji wa kijiji amekuwa akipewa taarifa juu ya kiwanda hicho na balozi na mwenyekiti wa kijiji lakini hakuna hatua yoyote ile aliyochukua jambo ambalo anatakiwa kukamatwa na kuhojiwa juu ya kiwanda hicho.

Biteko alisema Serikali imekuwa ikiboresha sekta ya madini kwa wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini wilayani Kahama lakini bado kuna baadhi yao wamekuwa wakiibia serikali mapato kwa kuanzisha viwanda bubu kwenye makazi yao watu.

“Kiwanda hiki kipo hapa katika nyumba hii tangu Julai mwaka jana huku kikiendelea kufanya kazi, Serikali imepoteza mapato mengi kwa kutochukua hatua za haraka, tutachukua hatua kali za kisheria kwa miliki wa mtambo huu na nyumba hii,” alisema Biteko.

Hata hivyo, Biteko aliwataka viongozi wa vijiji na mitaa wilayani hapa kuhakikisha wanawafichua wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu ya madini ambazo zinafanyika katika makazi ya watu na kuikosesha serikali mapato.

 

 

 

Pia, Biteko aliwaagiza viongozi wa mkoa wa Shinyanga kuthibiti vitendo vya biashara haramu ya madini vinaendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali na mpaka sasa wameshakamata viwanda bubu viwili vya uchenjuaji wa dhahabu.

Kwa upande wake, balozi wa kitongoji cha mnara wa voda, Masoud Bakari alisema alishatoa taarifa kwa mamlaka za kisheria  kuhusiana na uwapo wa kiwanda hicho katika eneo lake lakini hakuona hatua zozote zikichukuliwa kwa wahusika.

“Kiwanda hiki kipo katika nyumba hii tangu Julai mwaka jana, kuna vijana wanne ambao walikuwa wakifanya shughuli ya kuchenjua dhahabu hapa. Viongozi wote wa eneo hili wanajua na tumelalamika sana kuhusiana kumwagwa ovyo kwa maji yenye kemikali kwenye makazi yetu,” alisema Bakari.

Katika ziara hiyo, Biteko alikamata mifuko zaidi ya 35 ikiwa na Cabon zinadhaniwa kuwa na madini ya dhahabu katika kiwanda hicho huku mashine yenye uwezo wa kubeba kilo 500 za Cabon ikiwa tayari imewekewa mzigo kwaajili ya kuanza kazi.