VIDEO: Waziri Jafo aagiza walioenguliwa uchaguzi Serikali za Mitaa kurejeshwa

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania (Tamisemi) Selemani Jafo amewaagiza wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwarejesha wagombea wote waliochukua fomu na kufanikiwa kurejesha.

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania, Selemani Jafo amewarejesha wagombea wote wa Serikali za Mitaa ambao walichukua fomu na kurejesha.

Jafo ametangaza uamuzi huo leo Jumapili Novemba 10, 2019 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Hata hivyo, Jafo amesema uamuzi huo hautawahusu wagombea ambao si raia wa Tanzania na wale ambao hawajajiandikisha katika kijiji, mtaa ama kitongoji husika.

Wengine ambao hawahusiki ni waliojiandikisha kupiga kura mara mbili, waliojidhamini wenyewe, hajadhaminiwa na chama chake cha siasa, wamerejesha fomu watu zaidi ya mmoja kutoka chama kimoja kwa nafasi inayofanana ya mwenyekiti wa kijiji, mtaa au kitongoji kwa kijiji, mtaa, au kitongoji husika.

Ametaja  lingine ni mgombea aliyejitoa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Tangazo la Serikali Namba 3.71 la Mwaka  2019 kanuni ya 19.

Pia, waliojitoa kwa mujibu wa tangazo la Serikali Namba 372 la Mwaka 2019 Kanuni 20, Tangazo la Serikali Namba 373 la Mwaka 2019 kanuni ya 20 na Tangazo la Serikali Namba 374 la Mwaka 2019 Kanuni ya 20.