Waziri Mkuu kujulikana leo

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema leo Alhamisi Novemba 12, 2020 wabunge wataidhinisha uteuzi wa Waziri Mkuu baada ya jina lililoteuliwa na Rais John Magufuli kuwasilishwa bungeni.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema leo Alhamisi Novemba 12, 2020 wabunge wataidhinisha uteuzi wa Waziri Mkuu baada ya jina lililoteuliwa na Rais John Magufuli kuwasilishwa bungeni.

Ndugai amesema hayo leo wakati akitangaza shughuli zitakazofanyika katika kikao cha tatu cha Bunge leo akibainisha kuwa moja kati ya yatakayofanyika ni kuidhinishwa kwa jina hilo.

“Waheshimiwa wabunge karibuni sana, natumaini kila mmoja ameshaona orodha ya shughuli za leo ambazo ni muhimu sana. Ajenda itakayofuata ni uthibitisho ambao mtaufanya wabunge kwa uteuzi wa waziri mkuu.”

“Mkononi sina hilo jina lakini wakati ukifika mwakilishi wa rais utaruhusiwa kuingia hapa ndani na bahasha husika kwa hiyo nitakabidhiwa hapa mbele waheshimiwa”

Ndugai amesema kuwa shughuli ya kwanza ni kiapo kwa wabunge ambao hawajala kiapo, ikifuatiwa na kuidhinisha jina la waziri mkuu na mwisho kutakuwa na uchaguzi wa naibu spika wa Bunge.

Baada ya wabunge kuapishwa Spika Ndugai alitoa dakika 30 za mapumziko kwa wabunge kabla ya kuanza shughuli ya kuthibitisha uteuzi wa Waziri mkuu.