Yaliyotikisa kesi ya mauaji ya RPC Barlow

Muktasari:

Serikali ilikuwa na mashahidi 36, lakini ikawatumia 25 baada ya kuridhika na ushahidi wao


Mauaji ya Kamanda Liberatus Bar-low yalitokea Oktoba 13, 2012 katika eneo la Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.


Watu kadhaa walishikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, lakini baada ya uchunguzi wa kina, saba walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia na hatimaye Novemba 12, 2019 wanne walitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa huku watatu wakiachiwa huru.

Mwanza. Kuanzia mwishoni mwa Machi 2019, kesi namba 192/2014 ya mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow ilianza kuunguruma Mahakama Kuu.

Kamanda Barlow aliuawa Oktoba 13, 2012 katika eneo la Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Usikilizwaji wa kesi hiyo ambayo ilivutia na kufuatiliwa na wengi kila ilipokuwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa, ulihitimishwa Jumanne kwa hukumu iliyoshuhudia washtakiwa wanne wakihukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Washtakiwa watatu kati ya saba waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka hayo waliachiwa huru baada ya ushahidi kutowatia hatiani.

Waliotiwa hatiani ni Peter Muganyizi, Magige Mwita, Abdallah Petro na Abdulrahaman Ismail.

Washtakiwa wengine Chacha Mwita, Buganizi Edward na Bhoke Marwa waliachiwa huru.

Kesi hiyo ya mauaji iliibua mtikisiko kwa Jeshi la Polisi na jamii ndani na nje ya mkoa kutokana na nafasi ya Kamanda Barlow na mazingira ya tukio.

Idadi, taaluma, vyeo na hoja za mashahidi

Kwa mujibu wa wakili wa Serikali Robert Kidando, upande wa mashtaka awali ulipanga kuita mashahidi 36 kuthibitisha kosa dhidi ya washtakiwa, lakini uliishia kuita mashahidi 25 pekee baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa.

Kisheria, kila ushahidi ni muhimu na una nafasi yake katika kuthibitisha kosa na kuishawishi mahakama, lakini kuna ushahidi na mashahidi wanaoonekana kuwa msingi wa kesi.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika kesi hii ya mauaji ya Kamanda Barlow baada ya upande wa mashtaka kuwatumia wataalamu wa alama za vidole na milipuko kuthibitisha ushiriki wa washtakiwa.

Miongoni mwa wataalamu waliotoa ushahidi mbele ya Jaji Matupa ni pamoja na sajenti Hassan Wasoro, ambaye ni mchunguzi wa alama za vidole.

Sajenti Wasoro, aliyelazimika kuitwa mara mbili tofauti kutoa ushahidi, aliieleza mahakama kuwa alama za vidole vya washtakiwa vilioana na vilivyokutwa kwenye gari alilokuwa akiendesha Kamanda Barlow siku ya tukio, hivyo kudhihirisha kuwa walikuwepo eneo hilo na waliligusa gari hilo.

Mchunguzi wa bunduki

Ushahidi wa mkaguzi wa polisi, Gilbert Lukaka kuhusu bunduki na maganda ya risasi yaliyookotwa eneo la tukio, pia ulitumiwa na upande wa mashtaka kuthibitisha kosa dhidi ya washtakiwa.

Shahidi huyo wa 19, ambaye wakati anatoa ushidi wake alikuwa makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, aliiambia mahakama kuwa ujuzi, utaalamu na uzoefu wake wa kuchunguza bunduki na maganda ya risasi ulithibitisha kuwa maganda yaliyookotwa eneo la tukio yalioana na bunduki ambayo washtakiwa walidaiwa kuitumia kumuua Kamanda Barlow.

Ushahidi kamishina

Katika kuhakikisha unawatia hatiani washtakiwa, upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili Kidando akisaidiwa na mawakili Ajuaye Bilishanga na Levina Tibilengwa uliwaita mashahidi wenye vyeo vya juu akiwemo Kamishina wa Polisi, Robert Mayala.

Akiwa shahidi wa 20 katika shauri hilo, Kamishina Mayala aliiambia Mahakama mbele ya Jaji Matupa kuwa aliyekuwa mshtakiwa wa tatu katika shauri hilo, Magige Mwita alimwelezea jinsi mauaji ya Kamanda Barlow yalivyotekelezwa.

Endelea kufuatilia majukwaa na magazeti ya Mwananchi kupata mfululizo wa makala kuhusu ushahidi hadi hukumu ya kesi ya mauaji ya Kamanda Barlow.