Ziara ya Dk Bashiru Dar yaondoka na katibu, diwani wa Chadema

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ameendelea na ziara ya kukagua uhai wa chama hicho katika majimbo ya Dar es Salaam ambapo viongozi wa Chadema jimbo la Kawe wamekihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema Jimbo la Kawe Dar es Salaam kimepata pigo baada ya  Diwani wake wa viti maalum, Carolina Kazinza na Katibu wa jimbo hilo, Andrew Samsoni kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wanachama hao wamejiunga na chama hicho leo Jumapili Septemba 1, 2019 wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ya kukagua uhai wa chama sambamba na ufunguzi wa mashina katika majimbo ya Jiji la Dar es Salaam.

Wengine waliojiunga na CCM  ni pamoja na aliyekuwa Diwani wa Makongo, Deusdedit Mtilo na mwanasheria wa kanda ya Pwani wa Chadema, Nadia Karama.

Akizungumza kwenye mkutano wa ndani, Andrew amesema hawezi kuwa mnafiki kutokana na kazi zinazifanywa na Rais John Magufuli wa Tanzania.

Amesema yenye ndiye aliyeleta madiwani na mbunge wa jimbo la kawe  (Halima Mdee-Chadema) hivyo ameamua kurudi  mwenyewe kwa maslahi ya Taifa.

"Mimi ndiye niliyemchukulia Mdee fomu ya ubunge, nimerudi mwenyewe bila kushawishiwa na mtu yoyote kutokana na kazi anazozifanya Mheshimiwa Rais," amesema Samson