Zitto achukua fomu kutetea nafasi yake ACT-Wazalendo

Mwananchama wa Chama Cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akionyesha fomu ya kuwania nafasi ya Kiongozi wa Chama baada ya kukabidhiwa na  Mratibu wa Uchaguzi,  Risasi Semasaba katika makao makuu ya Chama hicho Kijitonyama jijini, Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe leo Jumanne, Februari 18, 2020 amechukua fomu ya kutetea nafasi yake ndani ya chama hicho.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe amechukua fomu  kutetea nafasi yake ndani ya chama hicho.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amechukua fomu leo Jumanne Februari 18, 2020 muda mfupi baada ya kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili. Katika shauri hilo la uchochezi Zitto amekutwa na kesi ya kujibu.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Zitto amesema ameamua kutetea nafasi hiyo kwa awamu ya pili baada ya kushauriana na watu mbalimbali ikiwemo familia yake.

 “Nimechukua tena fomu ya kugombea uongozi wa chama katika uchaguzi utakaofanyika katika mkutano wa chama utakaoanza Machi 14 hadi 16, 2020.”

“Mimi nimeshatumikia muhula mmoja na kwa mujibu wa Katiba yetu mihula ni miwili, kwa hiyo naomba muhula huu wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa katiba ya ACT-Wazalendo,” amesema Zitto.

Amewataka wanachama wengine kujitosa kuwania nafasi mbalimbali kwa kuwa hakuna nafasi ya mtu ndani ya chama hicho.

Zitto amekuwa kiongozi wa chama hicho tangu Machi 25, 2015.