Zitto ataka wapinzani kuungana 2020, ajipigia debe urais

Muktasari:

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema lazima vyama vya upinzani viungane katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, vikiona anatosha kuwania urais atakubali.

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema lazima vyama vya upinzani viungane katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, vikiona anatosha kuwania urais atakubali.

Zitto ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 5, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano  katika kipindi cha Konani cha kituo cha televisheni cha ITV wakati akijibu maswali ya mtazamaji aliyetaka kujua kama ana nia ya kugombea urais kwenye uchaguzi ujao.

Zitto amesema kwa muda mrefu amekuwa na nia ya kuwa Rais wa Tanzania, kusisitiza kuwa suala hilo si la mtu mmoja bali ni uamuzi wa chama au vyama vya siasa.

 “Iwapo vyama vitaona mimi ndiyo mgombea ninayestahili kupeperusha bendera nitagombea lakini vikiona mtu mwingine ndio anafaa zaidi basi nitamuunga mkono. Lazima tushirikiane kuiondoa CCM madarakani,” amesema Zitto.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo) amesema anaumizwa kuona takribani Watanzania milioni 14.7 wanaishi katika umasikini licha ya wingi wa rasilimali zilizopo. Amesema akiwa Rais atasimamia zaidi sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaajiri watu wengi.

Amesema Serikali haijawahi kutenga hata asilimia tatu ya bajeti yake kwenye sekta ya kilimo, hakuna mradi hata mmoja wa kilimo cha umwagiliaji ambao umezinduliwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Amesema mpaka sasa Tanzania ina hekta 400,000 tu za kilimo cha umwagiliaji.

Mwanasiasa huyo amesema akiwa Rais atahakikisha sera za uchumi zinamnufaisha Mtanzania kwa kuweka mipango ya kiuchumi itakayokuza uchumi wa Tanzania badala ya kupeleka fedha nje kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa.

“Wananchi wamejaa hofu, hawana furaha, wamekasirika muda wote. Wanahitaji wa kuwafanya wawe na furaha muda wote, ndiyo maana ninasema kwangu mimi itakuwa ni kazi na bata, tunafanya kazi ili tufurahi,” amesema Zitto.