kusuasua usajili laini za simu kwazua jambo, Majaliwa aionya Nida

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kufanya shughuli zao kikamilifu kuondoa malalamiko ya wananchi wanaoshindwa kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole kutokana na kutokuwa na vitambulisho vya uraia.

Geita. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kufanya shughuli zao kikamilifu kuondoa malalamiko ya wananchi wanaoshindwa kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole kutokana na kutokuwa na vitambulisho vya uraia.

Ili uweze kusajili laini ya simu ni lazima uwe na kitambulisho hicho kinachotolewa na Nida.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 21, 2019 katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Geita baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku Musukuma

Mbunge huyo amesema kuna hatari ya kutowasiliana  na wananchi wa jimbo lake kama watashindwa kusajili laini zao hadi mwisho wa usajili Desemba 31, 2019.

Msukuma alimuomba Majaliwa kuiagiza Nida kurudia usajili na kutoa namba za vitambulisho ili wananchi waweze kusajili laini zao.

Akizungumzia suala hilo, Majaliwa amesema haridhishwi na utendaji wa Nida kutokana na malalamiko anayoyapokea kutoka kwa wananchi kila anakopita.

Amemtaka mkurugenzi wa mamlaka hiyo kuhakikisha wananchi wote waliosajiliwa wanapewa namba za vitambulisho na kuwataka waanze tena uandikishaji ili waliopitwa na zoezi hilo kupata fursa.